Waasi wa Mali wajiondoa katika mchakato wa amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waasi wa Mali wajiondoa katika mchakato wa amani

Waasi wa kundi la Tuareg na muungano wa waasi wa kiarabu wametangaza kujiondoa katika mazungumzo na serikali ya Mali.Hii ni pigo kubwa kwa rais wa nchi hiyo Ibrahim Boubacar Keita anayejaribu kulinganisha taifa hilo

Taarifa ya pamoja kutoka kwa kundi la Tuareg na muungano wa waasi wa kiarabu imesema kufuatia matatizo chungu nzima katika utekelezaji wa makubaliano ya Ougadugou ambayo yanasababishwa na kushindwa kwa upande wa serikali kuheshimu mkataba huo,makundi hayo ya waasi yamejiondoa kutoka mchakato huo wa kutafuata amani nchini Mali.

Mkataba uliotiwa saini mwezi Juni mwaka huu katika nchi jirani ya Burkina Faso ulitoa fursa kwa jeshi la Mali kurejea katika mji mkuu wa jimbo la Kidal miezi 18 baada ya jeshi hilo kuutoroka mji huo kufuatia mashambulio makali kutoka kwa waasi.

Mapatano hayo ya Ougadougou yaliyomaliza mapigano ya miezi 18 nchini humo pia yalitoa fursa ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu mwezi Juni ambao Rais Keita alishinda.

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita

Hata hivyo kumekuwa na dalili za mvutano kati ya pande hizo mbili.Mapema mwezi huu wanajeshi wa Mali walikabiliana na waasi wa kituareg karibu na mpaka wa Mauritania,makabiliano ya kwanza kati yao tangu kutiwa saini mkataba huo wa amani.

Kupatikana amani sasa kwatiliwa shaka

Chini ya mkataba huo,mazungumzo ya kutafuata amani yalipaswa kuanza mwishoni mwa mwezi Novemba kati ya serikali na waasi wa muungano NMLA ambao wanataka kujitenga na kuunda taifa jipya la Azawad, na makundi mengine mawili ya waasi ambayo pia yametangaza kujiondoa kutoka mkataba huo.

Muasisi wa NMLA Mossa Ag Acharatoumane ameishutumu serikali kwa kushindwa kutimiza upande wake wa makubaliano hayo baada ya jeshi kukubaliwa kuingia maeneo ya waasi.

Kufuatia mkutano mjini Ouagadougou,makundi manne ya waasi yamesema yanataka mkutano wa dharura wa pande zote husika ili kutathimini utekelezwaji wa makubaliano ya Ouagadagou.

Wajumbe wa waasi na serikali ya Mali mjini Ouagadougou

Wajumbe wa waasi na serikali ya Mali mjini Ouagadougou

Waasi hao wanaotaka kujitenga kwa eneo la kaskazini mwa Mali miongoni mwa masuala mengine wanaishutumu serikali kwa kukosa kuwaachilia wafungwa kama walivyokubaliana.

Serikali ya Mali haijatoa tamko lolote kuhusiana na uamuzi huo wa waasi ambao unahofiwa huenda ukaibua hali mpya ya mivutano.Wiki iliyopita waandmanaji katika mji wa Kidal waliwarushia mawe maafisa wa serikali mpya waliokuwa wameuzuru mji huo.

Waasi kutoka kabila la Tuareg wamekuwa wakitaka kujitenga kwa eneo hilo la kaskazini tangu Mali kujinyakulia uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960 na mwaka jana waliongoza uasi mkubwa uliosababisha machafuko mabaya kiasi cha Ufaransa kutuma jeshi lake kudhibiti hali ya mambo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap/reuters

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com