Waasi wa M23 waionya Tanzania | Matukio ya Afrika | DW | 13.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waasi wa M23 waionya Tanzania

Waasi wa kundi la M23 wameitaka Tanzania kuachana na mipango ya kuchangia wanajeshi wake katika kikosi cha Umoja wa Mataifa kinachopangwa kutumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kupambana na waasi .

Waasi wa M23 Congo.

Waasi wa M23 Congo.

Waasi wa kundi hilo la M23 ambao wamekanusha madai ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwamba nchi jirani za Rwanda na Uganda zinawaunga mkono,wameonya katika baruwa iliyotumwa na kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo Betrand Bisimwa kwa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwamba daima wamekuwa wakipata ushindi dhidi ya vikosi vikubwa vyenye silaha nzuri.

Bisimwa ameandika " Jambo kama hilo litawakuta kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa cha kuingilia kati iwapo busara yao itashindwa kufanya kazi kuingilia kati na kuzuwiya hali ya hatari ilioko kwenye mkondo huo."

Bisimwa amesema kwa ajili hiyo kundi hilo la waasi la M23 linaomba bunge na wananchi wa Tanzania kufikiria upya kwa uangalifu juu ya hali hiyo na kuishawishi serikali ya Tanzania kutowapeleka watoto wao wa kiume na wa kike wa taifa hilo la uadilifu kushiriki kwenye vita vya kipuuzi dhidi ya ndugu zao wa Congo.

M23 kujibu mapigo ikishambuliwa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania.

Hapo Ijumaa kundi hilo lilionya kwamba watalipiza iwapo watashambuliwa na kikosi cha kuingilia kati mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambacho kitakuwa sehemu ya Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kuleta Utulivu kikiwa na jukumu la kuwalinda raia.

Msemaji wa kundi hilo la waasi Vianney Kazarama aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wao kundi la M23 hawana haki ya kushambulia kikosi cha Umoja wa Mataifa lakini iwapo kikosi hicho kitawashambulia wana haki ya kuchukuwa hatua ambapo watalipiza na watajihami.

Hapo tarehe 28 mwezi wa Machi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limeidhinisha kuundwa kwa kikosi cha zaidi ya wanajeshi 2,500 kikiwa na mamlaka ya kufanya mashambulizi ya kuwalenga waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo eneo lenye utajiri wa madini ambalo limekumbwa na mzozo kwa zaidi ya miongo miwili.

Ni tangazo la vita

Waasi wa M23 wakiweka ulinzi wakati wa kuchaguliwa kwa Bisimwa kuwa kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo mwezi wa Machi 2013

Waasi wa M23 wakiweka ulinzi wakati wa kuchaguliwa kwa Bisimwa kuwa kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo mwezi wa Machi 2013

Siku chache baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa aliita hatua hiyo kuwa ni tangazo la vita wakati mazungumzo ya kutafuta amani kati ya kundi hilo na serikali yakiwa yanaendelea mjini Kampala Uganda. Madnodie Muonoubai msemaji wa Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kuleta Utulivu ambacho kitajumuisha kikosi kitakachotumwa Congo amesema idadi rasmi ya wanajeshi watakaounda kikosi hicho ni 3,069.

Afrika Kusini,Tanzania na Malawi vitachangia wanajeshi wao katika kikosi hicho ambapo kila nchi itatuma wanajeshi 850 wa nchi kavu na kufikisha jumla ya wanajeshi 2,550. Msemaji huyo ameongeza kusema kwamba wanajeshi waliobakia 519 watatawanya katika vikosi vya mizinga, vikosi maalum na vikosi vya upelelezi.Kikosi hicho kitaongozwa na generali wa Tanzania.

Afrika Kusini na mdahalo wa kutuma wanajeshi

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini akihutubia wakati wa misa ya kumbukumbu ya wanajeshi wake waliouwawa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini akihutubia wakati wa misa ya kumbukumbu ya wanajeshi wake waliouwawa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Suala la kutumwa kwa wanajeshi wa Afrika Kusini nchi za nje limezusha mjadala nchini humo kufuatia kuuwawa kwa wanajeshi wake 13 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwishoni mwa mwezi uliopita wakati waasi walipompinduwa Rais Francois Bozize.

Kundi la waasi wa M23 tayari limelitaka bunge la Afrika Kusini katika baruwa yao ya tarehe 3 Aprili kutochangia wanajeshi wake katika kikosi cha Umoja wa Mataifa kitakachotumwa Congo. Msemaji wa jeshi la Afrika Kusini Brigedia Generali Xolani Mabanga ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanavizingatia vitisho vinavyotolewa na kundi la waasi la M23 lakini wao sio wa kuamuwa iwapo wapeleke au wasipeleke wanajeshi hao na kwamba watapeleka wanajeshi watakapoagizwa na serikali lakini hakuna kitakachowarudisha nyuma au kuwafanya wahofu.

Amesema "Iwapo tutaweka wanajeshi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kama sehemu ya kikosi cha Umoja wa Mataifa,tutafanya hivyo. Mojawapo ya majukumu yetu ni kwenda vitani,kupigana vita na kushinda vita." Kundi la M23 lililopewa jina kutokana na makubaliano yake ya amani na serikali yaliosainiwa tarehe 23 mwezi wa Machi mwaka 2009, limeibuka kutokana na uasi jeshini wa jamii ya Watutsi hapo mwezi wa Aprili mwaka 2012 kwa misingi kwamba serikali haitekelezi makubaliano hayo.

Walinda amani na mamlaka ya kushambulia

Waasi wa M23 wakati walipouteka mji wa Goma.

Waasi wa M23 wakati walipouteka mji wa Goma.

Waasi hao waliuteka kwa muda mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini wa Goma mwezi wa Novemba mwaka jana. Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Raymond Tshibanda amesema kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa cha kuingilia kati mashariki mwa Congo kitawekwa kufikia mwishoni mwa mwezi wa Aprili lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanataraji kwamba itachukuwa wiki kadhaa kabla ya kuanza kufanya kazi.

Hii ni mara ya kwanza kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kupatiwa mamlaka ya kufanya mashambulizi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Amina Abubakar