Waasi Syria wataka sasa kuwekwa zoni za kutoruka ndege
1 Juni 2013Hususan baadhi ya waungaji mkono upinzani wanatoa wito kwa rais Barack Obama kuchukua hatua zaidi kupindukia ile ya kupeleka silaha tu kwa makundi maalum ya waasi yaliyochaguliwa, chaguo ambalo utawala huo unaripotiwa kuwa umo katika hali ya tafakari tangu ripoti kujitokeza mwezi uliopita kuwa jeshi la Syria limetumia silaha za kemikali dhidi ya waasi.
Kutokana na hali ya sasa ya udhaifu wa upinzani, wanadai kuwa , haina maana kwenda katika majadiliano mwezi huu mjini Geneva na wawakilishi wa serikali ya rais Bashar al-Assad , kama ilivyopendekezwa na Marekani na Urusi, bila kwanza kujaribu kubadilisha hali ya mambo katika vita.
Zoni za kutoruka ndege
Wengi wa waungaji mkono wa waasi wanadai kuwekwa zoni moja ama zaidi za kutoruka ndege katika anga ya Syria kuwalinda wapinzani na kuwaruhusu kuunda serikali mbadala katika ardhi ya Syria ambayo inaweza kuomba usaidizi zaidi wa kijeshi wa kuingilia kati kutoka mataifa ya magharibi pamoja na washirika wa Kiarabu.
Baada ya siku nane za mivutano ya kutaka udhibiti na kwamba hakuna mshindi wa wazi, upinzani nchini Syria unaonekana kuwa umegawika zaidi kuliko hapo kabla.
Waasi wapoteza imani
Ndani nchini Syria, waasi wanaopigana na utawala wa rais Bashar al-Assad na wanaharakati wanasema kuwa wamepoteza uaminifu kwa wapinzani wanaoishi uhamishoni ambao wanaonekana kuwa hawana uwezo wa kuzuwia jeshi ya serikali kusonga mbele.
Muungano wa kitaifa umekamilisha mkutano wake uliodumu kwa siku kadha nchini Uturuki siku ya Ijumaa ambapo ulishuhudia waasi kutoka Qatar na Saudi Arabia wakifikia muafaka dakika za mwisho hali iliyofikiwa kwa upatanishi chini ya mbinyo mkubwa.
Baada ya saa kadha za mivutano , mkuu wa muungano huo George Sabra alitangaza kupanuliwa kwa kundi hilo na kujumuisha wajumbe 51 wengine wapya,na kufikisha idadi ya wajumbe 114.
Hadi sasa muungano huo umekuwa na wajumbe wengi kutoka kundi la udugu wa Kiislamu linaloungwa mkono na Qatar , lakini Saudi Arabia ambayo ina nguvu katika eneo hilo inataka kupunguza ushawishi huo.
Kati ya wajumbe hao wapya , kiasi ya 10 wanahusika na mpinzani maarufu Michel Kilo, ambaye juhudi zake za kuingia katika muungano huo ziliungwa mkono na Saudi Arabia.
Urusi yaonywa
Wakati huo huo Ujerumani na Marekani zimeionya Urusi jana Ijumaa(31.05.2013) kutohatarisha mkutano uliopangwa kwa ajili ya amani ya Syria ama kubadilisha uwiano wa nguvu katika mashariki ya kati kwa kuupatia utawala wa rais Bashar al-Assad silaha za kisasa za ulinzi wa anga.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na waziri mwenzake wa Ujerumani Guido Westerwelle wamesema kupeleka makombora ya S-300 kutoka Urusi kwenda Syria kutarefusha vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe, kuzuwia juhudi za kuunda serikali ya mpito kwa njia ya mazungumzo na kuathiri maslahi ya Israel ya kimkakati.
Kerry amewaambia waandishi habari katika mkutano wa pamoja na Westerwelle baada ya mkutano wao katika wizara ya mambo ya kigeni. "Tunawaomba tena kutoathiri uwiano katika eneo hilo kwa mtazamo wa Israel," amesema. "silaha ambazo zitapelekwa kwa Assad hata kama ni mkataba wa zamani ama vinginevyo, una athari mbaya katika uwiano wa maslahi na uthabiti wa eneo lote na unaiweka Israel katika hali mbaya.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / afpe / ips
Mhariri : Bruce Amani