Waandamanaji warudi mitaani Burundi | Matukio ya Afrika | DW | 19.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waandamanaji warudi mitaani Burundi

Waandamanaji wameendelea kumiminika mitaani nchini Burundi wakimpinga Rais Pierre Nkurunziza anayepigania kugombea awamu ya tatu, licha ya vitisho vya kuandamwa na serikali.

Waandamanaji wakirudi mitaani katika mji mkuu wa Bujumbura licha ya vitisho vya serikali.

Waandamanaji wakirudi mitaani katika mji mkuu wa Bujumbura licha ya vitisho vya serikali.

"Hatutaacha kuandamana mpaka yeye aache kugombea mara ya tatu," waandamanaji walipiga kelele katika kiunga cha Nyakabiga, kiini cha machafuko ya wiki tatu sasa ambayo yanaonekana sasa kuchochea hofu za kuzuka tena mapigano ya kikabila katika nchi hiyo ndogo kwenye eneo la Maziwa Makuu.

Waandamanaji wanasema suala la Nkurunziza kugombea kwa mara ya tatu linavunja katika na mkataba wa amani uliokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi mwaka 2005.

Kundi la majenerali wa kijeshi, likiwa na madai hayo hayo dhidi ya rais huyo, lilijaribu na likashindwa kumpindua wiki iliyopita na hapo jana Jumatatu (18 Mei), serikali ikasema ingeliyachukulia maandamano yoyote baada ya hapo kuwa ni muendelezo wa mapinduzi hayo yaliyoshindwa. Lakini waandamanaji hao walisema walikuwa wanapingana na Nkurunziza na pia jaribio hilo la mapinduzi.

"Hatutaki mapinduzi ya kijeshi, hatutaki muhula wa tatu. Tutaendelea kuandamana hadi naye akatae kugombea muhula wa tatu," mmoja wa waandamanaji aliyesema anaitwa Jean-Paul, aliliambia shirika la habari la Reuters. Alikataa kutoa jina lake la ukoo akihofia vikosi vya serikali.

Tafauti jeshini

Wanajeshi watiifu kwa Rais Pierre Nkrunziza wakiongoza msafara wa kiongozi huyo wakati akirejea nchini Burundi baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi tarehe 17 Mei 2015.

Wanajeshi watiifu kwa Rais Pierre Nkrunziza wakiongoza msafara wa kiongozi huyo wakati akirejea nchini Burundi baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi tarehe 17 Mei 2015.

Hata hivyo, tafauti na jana ambapo makundi mawili ya wanajeshi nusura yarushiane risasi wenyewe kwa wenyewe wakipingana juu ya ikiwa watumie silaha za moto dhidi ya waandamanaji au la, katika maandamano ya leo polisi na wanajeshi walisimama tu upande wa pili wa mtaa wakiwaangalia waandamanaji bila kuchukuwa hatua yoyote kuwazuia au kuwachawanya.

Burundi, taifa masikini lenye raia milioni 10, bado linaendelea kujijenga upya kutokana na athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo viliangamiza watu wapatao 300,000.

Nchi jirani ya Rwanda, ambayo ina mchanganyiko sawa wa kikabila kati ya Wahutu walio wengi na Watutsi walio wachache, ilikumbwa na mauaji ya maangamizi mwaka 1994, ambapo watu 800,000, wengi wao Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani, waliuawa.

Nkurunziza anasema kushiriki kwake kwenye uchaguzi wa mwaka huu hakuvunji sharti la mihula miwili ya urais lililomo kwenye katiba, kwani muhula wake wa kwanza hauhisabiwi kwa sababu aliteuliwa na bunge na sio kuchaguliwa kwa kura ya wananchi.

Katika kile kinachoonekana kama hatua ya kuimarisha nguvu zake jeshini, jana Rais Nkurunziza alimfuta kazi waziri wake wa ulinzi, Pontien Gaciyubenge, ambaye mapema mwezi huu alikuwa amesema jeshi lisingeliegemea upande wowote na lingeendelea kuheshimu katiba, kauli ambayo ilichukuliwa kama ni kumkosoa rais huyo.

Vile vile, Nkurunziza alimuondoa waziri wake wa mambo ya ndani, Laurent Kavakure, na wa biashara, Marie Nizigiyimana.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman