Waandamanaji wachoma majengo Misri | Matukio ya Afrika | DW | 10.03.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waandamanaji wachoma majengo Misri

Waandamanaji wa Misri wamechoma moto majengo mjini Cairo, na kujaribu bila mafanikio kuvuruga usafiri wa meli katika mto Suez, wakati hukumu ya mahakama katika vurugu za soka ilipochochea hasira.

[38024942] Clashes in Cairo following Port Said trial verdict Ofisi za shirikisho la mpira wa miguu mjini Cairo zikiwaka moto.

Ofisi za shirikisho la mpira wa miguu mjini Cairo zikiwaka moto.

Hukumu hiyo iliwakasirisha wakaazi wa mji wa Port Said, katika lango la kaskazini la mto Suez, kwa kuthibitisha adhabu ya kifo waliopewa mashabiki 21 wa eneo hilo, kutokana na ushiriki wao katika vurugu mwaka uliyopita, zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya 70. Lakini mahakama hiyo pia iliwaudhi mashabiki hasimu mjini Cairo, kwa kuwaachia huru washtakiwa wengine 28, ambao wao waliitaka mahakama iwadhibu, wakiwemo maafisa saba wa jeshi la polisi, linalochukiwa na jamii kutokana na matumizi ya nguvu iliyopitiliza chini ya utawala wa rais aliepinduliwa Hosni Mubarak.

Majaji wa mahakama ya uhalifu ya Port Said wakisikiliza kesi za vurugu za mpira mjini Cairo kwa sababu za kiusalama. Mahakama ya Cairo ilithibitisha adhabu ya kifo kwa mashabiki 21 wa timu ya Al-Masry ya mjini Port Said.

Majaji wa mahakama ya uhalifu ya Port Said wakisikiliza kesi za vurugu za mpira mjini Cairo kwa sababu za kiusalama. Mahakama ya Cairo ilithibitisha adhabu ya kifo kwa mashabiki 21 wa timu ya Al-Masry ya mjini Port Said.

Duru za usalama zilisema watu wawili, mwanaume alie katika umri wa miaka 30 na mvulana mdogo walifariki mjini Cairo kutokana na athari za gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira. Jumla ya watu 65 walijeruhiwa. Maandamano hayo ya Jumamosi yalitilia msisitizo namna rais Mohammed Mursi anaendelea kupambana, miaka miwili baada ya kunagushwa kwa Hosni Mubarak, kulinda usalama na utulivu katika wakati wa migogoro ya kiuchumi na kisiasa.

Makundi ya Kiislamu yanayomuunga mkono rais Mursi yameonya dhidi ya kuvunjika kwa hali ya usalama na kuwataka wafuasi wake kuunda kamati za ulinzi kulinda mitaa na mali za umma, iwapo jeshi la polisi litashindwa kufanya hivyo. Ofisi ya rais ilisema katika taarifa kuwa maandamano hayo hayakuwa ya amani na kulaani uharibu wa mali. Baraza la mawaziri nalo lilitoa taarifa kama hiyo, na kuwataka raia wa Misri kuungana na kuheshimu maamuzi ya mahakama.

Siku ya Alhamis kamati ya uchaguzi ilifuta ratiba ya uchaguzi wa wawakilishi wa baraza la chini la bunge, uliyokuwa uanze mwezi ujao, kufuatia amri ya mahakama iliyoutupa mchakato mzima wa uchaguzi katika wahka. Vurugu za uwanjani zilitokea mwaka uliyopita, mwishoni mwa mechi kati ya timu wenyeji Al-Masry na ile ya mjini Cairo Al-Ahly. Watazamaji walikanyagwa baada ya makundi yaliyoingiwa na hofu kujaribu kutoroka kutoka uwanjani humo, kufuatia uvamizi wa mashabiki wa klabu ya Al-Massry.

Kifo kwa kunyongwa

Jaji Sobhy Abdel Maguid, akiyaorodhesha majina ya mashabiki 21 wa Al-Masry, alisema mahakama ya mjini Cairo ilithibitisha adhabu ya kifo kwa kunyongwa. Pia aliwahukumu watu wengine watano kifungo cha maisha jela, wakati wengine kati ya jumla ya watu 73 walipata vifungo vifupi. Mjini Cairo, mashabiki wa klabu ya Al-Ahly waliokasirishwa na hukumu, waliichoma moto klabu ya polisi, ofisi ya karibu ya shirikisho la mpira wa miguu ya Misri, na tawi la mgahawa, na kupelekea moshi kutanda katika anga ya mji mkuu.

'Mashabiki waliopitiliza', ambao ni sehemu ya wafuasi wa klabu ya Al-Ahly wanaohusika na vurugu nyingi zaidi, walisema walitarajia adhabu inayostahili kwa watu waliopanga mauaji ya Port Said. Kundi hilo lilisema katika taarifa yake kuwa kilichotokea siku ya Jumamosi ni mwanzo tu wa hasira, na kuongeza kuwa kama wahusika wengine wa mauaji hayo hawatabainishwa, machafuko zaidi yatatokea.

Mashabiki wa klabu ya Al-Ahly, maarufu kama Ultras wakiandamana mbele ya klabu yao baada ya kutolewa hukumu ya mwisho katika kesi hiyo.

Mashabiki wa klabu ya Al-Ahly, maarufu kama "Ultras" wakiandamana mbele ya klabu yao baada ya kutolewa hukumu ya mwisho katika kesi hiyo.

Mjini Port Said, ambako jeshi lilichukuwa jukumu la ulinzi kutoka kwa Polisi siku ya Ijumaa, karibu wakaazi 2,000 waliotaka mashabiki waondolewe adhabu ya kifo walizuia feri kuvuka mto Suez. Mashu walisema vijana walizifungulia boti zilizotia nanga, ambazo zinatoa huduma katika mto huo, wakitumaini zingezuia njia ya meli zinazopita. Jeshi liliokoa boti tano za kasi na kuzirudisha nchi kavu, lakini mbili zilikuwa bado zinaelea, alisema shuhuda mmoja.

Msemaji wa mamlaka ya mto Suez Terek Hassanein aliliambia shirika la habari la nchi hiyo MENA, kuwa usafiri wa meli zinazopita katika mto huo haukuathirika.

Uungwaji mkono wa makundi ya Kiislamu

Hazem Salah Abu Ismail, mhadhiri maarufu wa Salafi, alilaani majaribio ya wapinzani na makundi ya vijana kwa kuihujumu nchi kwa lengo la kuweka ombwe la uongozi, na kurejesha utawala wa kijeshi. "Tutakabiliana na majaribio yote ya upinzani...kurejesha utawala wa kijeshi, tuna makundi maarufu ya kulinda," alisema Ismail.

Vyama vya Salafi Al-Nour na Gama'a al-Islamiyya, vilivyolaumiwa kwa kufanya vurugu nchini Misri katika miaka ya 1990, vilitoa taarifa kama hizo, vikitoa wito kwa wafuasi wake kuchukua nafasi ya jeshi la polisi, kama jeshi hilo litaamua kuondoka mitaani.

Jenerali Ahmed Wasfy, ambae anaongoza jeshi katika mji wa Port Said alikataa wito wa kurejea katika utawala wa kijeshi. Jeshi linadhibiti usalama katika mji wa Port Said na miji mingine iliyoko kandoni mwa mto Suez. "Vikosi vya ulinzi vya Misri ni taasisi ya mapambano na si ya ulinzi, hakuna anaeweza kufikiri kuwa jeshi litachukua nafasi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi," alinukuliwa na shirika la MENA akisema.

Wamisri wakiimba juu ya gari la jeshi, baada ya jeshi kuchukuwa jukumu la ulinzi mjini Port Said, baada ya polisi kuanza kuogmea majukumu yao.

Wamisri wakiimba juu ya gari la jeshi, baada ya jeshi kuchukuwa jukumu la ulinzi mjini Port Said, baada ya polisi kuanza kuogmea majukumu yao.

katika tishio tofauti la kiusalma, wizara ya mambo ya ndani imeliagiza jeshi la polisi katika rasi ya Sinai kuongeza tahdhari, baada ya kupokea taarifa za kiintelijensia kuwa wapiganani wa jihadi wanaweza kuwashambulia, liliripoti shirika la MENA. Maafisa wameelezea wasiwasi kuhusu hali ya usalama katika eneo hilo la jangwa, ambalo linapakana na Israel, na lina maeneo kadhaa ya kitalii.

Alhamisi wiki iliyopita, watu wenye silaha waliwashikilia kwa muda, mkuu wa kampuni ya mafuta ya Marekani ExxonMobil nchini Misri na mke wake. Waingereza hao waliokuwa wakielekea katika moja ya maeneo ya mapumziko mjini Sinai, waliachiwa wakiwa salama.

Misri inakabiliwa na machafuko wakati ambapo maskini wa nchi hiyo wanateseka kutokana na mgogoro wa kiuchumi. Hifadhi ya fedha za kigeni imeshuka kwa kiwangi kikubwa, na sasa zinazidi kidogo tu ya theluthi moja ya kiwango cha wakati alipoondoka Hosni Mubarak. Sarafu ya Misri pauni imeshuka kwa asilimia 14 ikilinganishwa na dola ya Marekani tangu mapinduzi ya mwaka 2011, na nakisi ya bajeti inaongezeka kwa viwango vya kutisha kutokana na gharama za mafuta na ruzuku za chakula.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre

Mhariri: Amina Abubakar