Vyama vya Tshisekedi, Kabila vyaanza kuvutana | Matukio ya Afrika | DW | 10.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

DRC

Vyama vya Tshisekedi, Kabila vyaanza kuvutana

Umeibuka mvutano baada ya ziara ya Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini Marekani ambako alisema anataka msaada wa kungo’a mizizi ya udikteta nchini mwake.

Mwandishi wa DW mjini Kinshasa anasema chama cha FCC kililezea kuhuzunishwa kwake na matamshi hayo ya Rais Tshisekedi akiwa Washington wiki iliyopita.

Tshisekedi alisema ameomba msaada wa Marekani ili kungo’a mizizi ya udikteta wa serikali iliyopita. 

Kwenye taarifa iliyotolewa na chama hicho cha rais wa zamani, Joseph Kabisa, kilisema "matamshi hayo hayatochangia kuweko na mshikamano wa kitaifa kwenye serikali ya mseto."

Chama hicho pia kilikosoa vikali matumizi ya fedha za umma yaliyofanywa na Rais Tshisekedi mnamo kipindi cha miezi miwili tu ya utawala wake.

Wadadisi wa mambo wanasema ushirikiano wa chama cha Tshisekedi na kile cha Kabila hauwezi kudumu daima kutokana na tofauti kubwa za kimiitizamo.

Tshisekedi agoma kumteuwa waziri mkuu wa Kabila

Katika hatua nyengine, duru za kuaminika zinaelezea kwamba Rais Tshisekedi amekataa katakata kumteuwa waziri mkuu aliyependekezwa na Kabila.

Alebert Yuma, ambaye ni mshirika wa karibu wa Kabila, alitakiwa kuteuliwa kuwa waziri mkuu, lakini Tshisekedi hadi sasa bado hajatangaza jina lake.

New York Besuch Kongo Präsident Felix Tshisekedi bei Pompeo (Getty Images/AFP/A. Caballero-Reynolds)

Rais Felix Tshisekedi wa Kongo (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, wakati wa ziara ya Tshisekedi nchini Marekani tarehe 3 Aprili 2019.

Duru kutoka ikulu zinaelezea kwamba Tshisekedi ameomba apewe jina jengine, kwani Yuma, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya madini iitwayo GECAMINES, hana sifa nzuri ya uongozi.

Wakati huo huo, uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Machi, ulifanyika siku ya Jumatano (10 Aprili), huku matokeo yake yakitarajiwa jioni ya siku hiyo.

Uchaguzi huo wa magavana ulijumuisha majimbo 24 miongoni mwa 26 ya Kongo, huku ule majimbo mawili ya Kivu ya Kaskazini na na Maindombe uchaguzi ukiahirishwa hadi Mei 30.

Katiba ya Kongo inaelezea kwamba ni wabunge wa majimbo ndio wanaochaguwa maseneta pamoja na magavana wa majimbo.

Awali, tuhuma za rushwa zilipelekea uchaguzi huo wa magavana kuahirishwa mwezi Machi na kusababisha maandamano ya wafuasi wa chama tawala cha UDPS kufuatia matokeo ya uchaguzi wa maseneta.


Imetayarishwa na Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa