1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita ya kumaliza nne bora na ya kuepuka kushuka daraja

Admin.WagnerD17 Mei 2021

Ilikuwa ni wikiendi ya mshikemshike katika viwanja vya Bundesliga katika vita vya kujikatia tiketi za kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, na vya kuepuka kushuka daraja.

https://p.dw.com/p/3tV4T
Fussball Bundesliga l 1. FSV Mainz 05 vs Borussia Dortmund - Tor 0:3
Picha: Patrick Scheiber/Jan Huebner/Pool/imago Images

Borussia Dortmund na Wolfsburg zimefuzu katika Ligi ya Mabingwa baada ya kushinda mechi zao jana. Dortmund ilishinda 3 – 1 dhidi ya Mainz wakati Wolfsburg ikitoka sare ya 2 – 2 na RB Leipzig na kuhakikisha kuwa timu hizo zitamaliza katika nne bora na kucheza Champions League msimu ujao. Kiungo wa Dortmund Jude Bellingham alielezea furaha ya timu nzima "Tumefanya kazi kubwa sana katika mechi chache zilizopita kuweka mfululizo wa matokeo ya ushindi. Mwishowe tumestahiki. Nafikiria sana kuna watu waliotukatia tamaa. Tulikuwa na safari ndefu sana kutoka nafasi ya nne. Kuipata sasa huku kukiwa na mechi moja ya ziada ni ahueni kubwa kwetu."

Leipzig ambayo imekamata nafasi ya pili nyuma ya bingwa Bayern Munich, ilikuwa tayari imejihakikishia kandanda la Champions League msimu ujao.

Eintracht Frakfurt ilionekana kufuzu wakati ilikuwa mbele ya Dortmund kwa pengo la ointi saba zikiwa zimesalia mechi sita, lakini timu ikayumba baada ya kocha Adi Hutter kutangaza kuwa anaondoka kujiunga na Borussia Moenchengladbach msimu ujao. Kichapo cha Frankfurt cha 4 – 3 dhidi ya Schalke kilikuwa cha tatu katika mechi tano.

Kombibild l Gerd Mueller und Lewandowski
Lewandowski aifikia rekodi ya Gerd Mueller ya mabao 40 kwenye msimu mmoja wa Bundesliga

Lewandowski avunja rekodi

Ilikuwa wikiendi ambayo Robert Lewandowski aliifikia rekodi ya miaka 49 ya Gerd Mueller ya ufungaji mabao baada ya mshambuliaji hiyo wa Bayern Munich kufunga bao lake la 40 la Bundesliga msimu huu katika sare ya 2 – 2 dhidi ya Freiburg. Mpoland huyo aliifikia rekodi ya Mueller, aliyofunga kwenye mechi 34 katika msimu wa 1971/72, katika mechi 28 tu msimu huu. "Siwezi kueleza hasa kilichotokea katika mazingira haya, lakini labda haiwezekani kuvunja rekodi ya nguli kama huyo katika mechi moja.  Bado nna mechi moja iliyosalia na inapendeza sana kufikia kiwango cha Mueller na wachezaji wengine wengi bora. Inapendeza sana kuwa na nafasi ya kuandika rekodi nyingine na nitajaribu."

Katika mapambano makali ya kuepuka kushushwa daraja, Augsburg ilipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Werder Bremen ambao umeiweka katika eneo salama, lakini ukaitumbukiza Bremen katka nafasi hatari hali ambayo imesababisha klabu hiyo kumtimua kocha Florian Kohfeldt. Hertha Berlin pia wako salama baada ya sare tasa na Cologne, ambao wanahitaji ushindi katika siku ya mwisho dhidi ya Schalke ili kuwa na matumaini. Arminia Bielefield wako nje ya eneo la kushushwa daraja lakini huenda wakahitaji kittu dhidi ya Stuttgart katika siku ya mwisho kwa kutegemea watakachokifanya Werder Bremen dhidi ya Gladbach. Kwa timu hizo tatu, hatima yao itaamuliwa wikiendi ijayo ambayo ndio mwisho wa msimu.

AFP/Reuters/DPA/AP