Vita vya kikabila huko Darfur vyazusha hofu kubwa | Matukio ya Afrika | DW | 06.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Damu yamwagika tena Darfur

Vita vya kikabila huko Darfur vyazusha hofu kubwa

Watu wasiopungua 50 wameuwawa mpaka sasa katika vita vilivyoanza Jumamosi iliyopita katika mji mkuu wa Darfur Magharibi na hofu bado imetanda ingawa kuna utulivu wa kiasi.

Ni vita vilivyoanza kushuhudiwa kiasi siku nne zilizopita, katika mji wa El Geneina ambao ni mkuu wa Darfur Magharibi mwa Sudan na ulioko karibu kabisa na mpaka wa Chad. Vita hivyo vimehusisha silaha  ikiwemo risasi na makombora kwa mujibu wa wakaazi. Kamati ya madaktari wa eneo hilo imesema idadi walioikusanya mpaka hivi sasa ya waliouwawa ni watu 50 na waliojeruhiwa ni watu 132.

Kamati hiyo ya madatari kupitia taarifa walioitowa wameeleza kwamba hali ya utulivu kiasi ilirejea jumatatu usiku lakini bado timu ya madaktari bado inahofia kuendelea na shughuli zake.Shirika la uratibu wa  msaada wa kibindamu la Umoja wa Mataifa OCHA jana liliripoti kwamba waliouwawa ni watu 40 na wengine 58 wamejeruhiwa katika machafuko hayo ya kikabila kati ya jamii ya wenye asili ya kiarabu na wale wasiokuwa wa asili ya kiarabu wa kabila la Massalit.

Hii leo mkaazi mmoja kwa jina Mohammed Abdel-Rahman-wa El-Geneina kunakotokea mapigano hayo amezungumza na shirika la habari la AFP kwa njia ya simu na kusema kwamba hali ya utulivu ilikuwepo  usiku lakini leo asubuhi walisikia milia ya risasi kutoka upande wa wilaya ya Hay Al-Jabal ambayo ilidumu kwa takriban saa nzima.

Mkaazi mwingine anayekaa kilomita tatu kutoka hapo Hay Al-Jabal vilevile amesema kwao pia milio ya risasi ilisikika. Jumatatu usiku mamlaka nchini Sudan ilitangaza hali ya hatari na kupeleka wanajeshi Darfur Magharibi.

Aidha Umoja wa Mataifa ukatangaza kuzuia safari zake za ndege na shughuli zake zote za msaada katika mji unaokabiliwa na machafuko ambao ni kituo kikuu cha shughuli za msaada wa kiutu.Umoja huo wa Mataifa umesema uamuzi waliouchukua unaweza kusababisha athari kwa watu zaidi ya 700,000. Imeelezwa kwamba machafuko hayo yalizuka siku ya Jumamosi na watu chungunzima waliojeruhiwa wamepelekwa katika hospitali za mji mkuu wa Sudan Khartoum kwaajili ya matibabu ya dharura..

Sio mara ya kwanza machafuko kushuhudiwa katika mji huo,yamewahi kutokea mapigano  mnamo mwezi Januari mwaka huu wakati watu wa jamii ya kabila la Masalit kumuua mtu kutoka jamii ya  asili ya kiarabu.Wanamgambo walitumia tukio hilo kama sababu ya kuushambulia mji huo.

Lakini pia ikumbukwe kwamba jimbo la Darfur ni jimbo ambalo kwa miaka mingi linakabiliwa na machafuko. Yaliwahi kuzuka mapigano mwaka 2003 ya makundi mbali mbali ya waakazi wake wakidai kushirikishwa zaidi kisiasa na  serikali ya Sudan iliyokuwepo wakati huo chini ya rais Omar al Bashir. Na vikosi vya serikali na washirika wao kundi la wanamgambo wa asili ya kiarabu la Janjaweed waliwashambulia kikatili wakaazi wa jimbo hilo na kuua takriban watu 300,000.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Daniel Gakuba