Vita, njaa na mivutano ya kisiasa yaikabili Somalia | Matukio ya Afrika | DW | 03.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Somalia bado taabani

Vita, njaa na mivutano ya kisiasa yaikabili Somalia

Serikali mpya ya Somalia  imetakiwa kuhakikisha  kuwa vikosi vyake vya usalama vinawajibika na kuimarisha ulinzi hasa  miongoni  mwa watu wanaoshi katika mazingira hatari.

Katika ripoti yake iliyoangazia  maswala 10 yanayopaswa kupewa kipambauele, Somalia kuhusiana na haki za binadamu, Shirika la human rights watch limesema matatizo mengine yanapaswa kushughulikiwa kwa haraka pamoja na yale yanayotokana na  vita, njaa na mivutano ya  kisiasa. Tangu kuchaguliwa rais na wabunge na maseneta, Mohamed Abdullahi Farmajo amekabiliwa na changamoto chungu nzima katika kutafuta suluhu ya matatizo yanayoikabili Somalia.

Ugaidi, uchumi unaoyumba, uhaba wa chakula na mivutano ya kisiasa kati ya koo mbalimbali ni miongoni  tu mwa matatizo hayo. Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, uongozi mpya Somalia haujachukua hatua za haraka  kuwalinda raia  wote  hasa walio katika hatari ya kudhulumiwa kwa kuwachukulia hatua wahusika. Mapigano kati ya vikosi vya serikali  na wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab, pia yametajwa kuwaumiza zaidi raia.

The Wider Image: A daughter's freedom weighed against her siblings' lives (Reuters/Z. Bensemra )

Mama na wanawe katika kambi ya wakimbizi wa ndani Dollow,Somalia

Uchunguzi uliofanywa na Human rights Watch umebaini kuwa pande zote mbili, zimesababisha mauaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu miongoni mwa raia  katika maeneo wanayodhibiti.Serikali ya Somalia inapanga  kuimarisha operesheni zake za kijeshi ili kuwaangamiza kabisa wapiganaji wa kundi la al-shabaab, na hilo limelitia wasiwasi shirika la human rights watch huku  maafisa wake wakisema itakuwa muhimu kwanza  kuwepo utaratibu wa kuhakikisha kuzingatiwa nidhamu na kwa vikosi vya usalama kuwalinda raia dhidi ya dhulma.

Idara ya ujasusi nchini Somalia inadaiwa kuwanyima  wafungwa haki zao za kimsingi, kuwazuilia washukiwa kwa muda mrefu bila kuwafungulia mashtaka, kuwazuia kupata huduma za kisheria na  kuwatesa washukiwa ili kupata ushahidi. Mazungumzo yanayoendelea kwa sasa  kuhusu kuundwa mfumo wa kitaifa wa usalama  pia yanadaiwa kupuuza utendakazi wa  idara ya ujasusi.Katika miaka ya hivi karibuni, utawala nchini Somalia umetegemea  zaidi mahakama za kijeshi  kushughulikia  kesi mbalimbali  ambazo zinapaswa kushughuliwa na mahakama za kawaida kuanzia  kesi za ugaidi na nyingine nyingi  dhidi ya raia swala ambalo ni kinyume na sheria za kimataifa.

Kindersoldat vor Kämpfen in Somalia (picture-alliance/dpa/epa Albadri)

Mmoja wa watoto wanaotumiwa vitani

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human rights Watch  wahusika wote katika vita nchini Somalia pia wamekuwa wakiwatumia watoto walio chini ya umri wa miaka 18  katika vikosi vyao licha ya kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Huku pia taifa hilo  likikabiliwa na baa la njaa, serikali mpya imetakiwa  kutokiuka haki za  watu waliochwa bila makao  ikiwemo pia kutowafurusha kwa nguvu raia kutoka maeneo wanamoishi.

Mwandishi:Jane Nyingi/Human rights Watch
Mhariri:Josephat Charo