Viongozi wa magharibi wajadili mgogoro wa Sahel bila Waafrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa magharibi wajadili mgogoro wa Sahel bila Waafrika

Kwenye mkutano wa usalama wa Munich, mataifa makubwa ya magharibi yalieleza wasiwasi kuhusu hali ya usalama inayozidi kuzorota katika kanda ya Sahel, lakini viongozi wa Kiafrika walioalikwa walikwepa mkutano wa kilele.

Kwenye mkutano wa 56 wa usalama wa Munich nchini Ujerumani, mataifa makubwa ya dunia yaligeukia masuala ya ulinzi wa kimataifa - yakijikita juu ya kile kilichotajwa kama "westlessness" - ambayo ni dhana kwamba mataifa ya magharibi hayana uhakika kuhusu maadili yake na ulelewa wa mazingira yao ya kimkakati.

Maafisa pia walijadili athari za mripuko wa virusi vya Corona, Mashariki ya Kati na mzozo wa Libya. Katika Hoteli ya Bayerischer Hof iliyofurika, sura za kiafrika, wajumbe wa ngazi ya chini, walikuwa wanahesabika tu vidoleni. Hakuna hata kiongozi mmoja wa nchi kutoka bara hilo aliehudhuria, wakati ambapo kitisho kinaongezeka kuhusu ugaidi na mzozo ya kutumia silaha inayotishia kulisambaratisha bara hilo.

Deutschland München Sicherheitskonferenz MSC Bundespräsident Steinmeier

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akifungua mkutano wa usalama wa Munich, Februari 14, 2020.

Ripoti ya shirika la hisani la Save the Children ilichapishwa katika wakati ambapo viongozi wa dunia walikuwa wanakusanyika mjini Munich, Ujerumani. Tangu 2005, inasema ripoti hiyo, watu wasiopungua 95,000 waliuawa au kukatwa vioungo. Malefu walitekwa nyara, na mamilioni kunyimwa fursa ya kupata elimu.

Watoto wa Kiafrika ndiyo waliathirika zaidi, kwa mujibu wa Save the Children. Milioni 170 barani Afrika na Mashariki ya Kati wanaishi kwenye maeneo ya migogoro. "Utagundua kuwa mizozo yenye vurugu zaidi haionekani," anasema Dan Smith, Mkurugenzi wa SIPRI katika mazungumzo na DW. SIPRI ni shirika la ushauri la kimataifa linaloendesha utafiti juu ya migogoro, zana za vita, udhibiti wa silaha na upunguzaji wa silaha za vita.

Smith anaeleza kusikitishwa kwake na ukweli kwamba jamii ya kimataifa haitoi nadhari juu ya mgogoro unaofukuta barani Afrika. "Wao (Waafrika) siyo sehemu ya fikira ya jamii ya usalama iliyokusanyika hapa," anaongezeka Smith. "Hilo halimaanishi kwamba wasiwasi wa jamii hii hauna mashiko, lakini haujajikita juu ya kanda ya Sahel; haujajikita juu ya eneo la Pembe ya Afrika."

Wataalamu wa usalama wanasema Mataifa ya Magharibi hayajali kwa sababu kanda ya Sahel na migogoro ya silaha katika kanda ya Afrika Magharibi na Pembe ya Afrika iko mbali vya kutosha kutoka Ulaya kuweza kuwasababishia wasiwasi. "Jambo linapotokea katika kanda ya Sahel, kama halisababishi uhamiaji kuelekea Ulaya - Bara la Ulaya halijali hasa kuhusu hilo," anasema Smith.

Ujerumani yatoa hoja kuhusu Sahel

Wakati viongozi wa Kiafrika hawapo kuleta suala hilo mezani, waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer (AKK) alitoa wito wa kuongeza kuhudi za mapambano dhidi ya wapiganaji wa itikadi kali barani Afrika.

Zentral-Afrika Marie-Noëlle Koyara Verteidigungsministerin

Waziri wa ulinzi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Marie-Noelle Kayora.

"Kanda ya Sahel ni muhimu kwa Ulaya, kwa mfano, linapokuja suala la uhamiaji au kitisho cha ugaidi," alisema, na kuongeza kwamba, "ndiyo maana no muhimu kwa Ujerumani kuendelea kujitolea katika eneo hilo, kijeshi pia."

Tamko la AKK lilimhamasisha waziri wa ulinzi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Marie-Noelle Koyara. "Natumia fursa hii kuishukuru serikali ya Ujerumani kwa kufanya uamuzi wa busara kama huo," Koyara aliiambia DW. Kwa sababu anasema, mbali na masuala ya kisiasa - ni muhimu kujali pia kuhusu utu.

Jamhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu 2012. Kundi la waasi ambao wengi wao walikuwa Waislamu la Seleka lilitwaa madaraka mjini Bangui mwaka 2013. Tangu wakati huo taifa hilo limeshuhudia mauji ya maelfu katika mapigano kati ya makundi ya Kikristo na Kiislamu.

"Ukiwatazama watoto milioni moja wanaoteseka, wanawake wanaokimbia kimbia kunusuru maisha yao, wanawake wanaobakwa na vijiji vizima vinavyoripuriwa, ubinadamu hauwezi kuvumilia hayo," Koyara aliunga mkono wito wa Ujerumani wa kuchukuliwa hatua katika maeneo ya Afrika yaliosambaratishwa na vita.

Benki ya Dunia yaongeza msaada

Mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi ulioangulia mkutano wa usalama wa Munich, uliwakumbusha magwiji wa usalama na siasa mjini Munich kwamba vita vya Darfur - vilivyotokea miaka 17 iliyopita - vilisababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na baadae kugharimu maisha ya watu 300.000.

München Sicherheitskonferenz Bayern MSC

Hoteli ya Bayerischer Hof, unakofanyika mkutano wa usalama wa Munich.

Mgogoro huo umechochea uharibifu wa mazingira nchini Sudan, na kuwalaazimu zaidi ya watu milioni kuishi kwenye kampi za wakimbizi. Hii leo, migogoro inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi inasambaa haraka katika eneo la Sahel.

Watu milioni 4.2 wamepoteza makaazi yao kufikia Machi 2019. Idadi hii ni milioni moja zaidi ya idadi iliyorekodiwa mwaka 2018. Vurugu ziliongezeka mwaka 2019 -- hasa nchini Mali, Burkina Faso, Niger, na maeneo yanayozungunza Ziwa Chad.

Katika kuitikia mgogoro huo, Benki ya Dunia inamtuma mkurugenzi wake wa operesheni, Axel van Trotsenburg, kwenda katika kanda hiyo. "Tunapanga, katika miaka mitatu ijayo, kutoa kiasi cha dola bilioni 53 kwa kanda ya Afrika," alisema kuelekea safari yake nchini Burkina Faso, Mali, Chad na Mauritania. " Nadhari makhsusi itatolewa kwa mataifa yalio katika hali tete kwenye kanda ya Sahel, eleo la pembe ya Afrika na Ziwa Chad," Van Trotsenburg aliimabia DW.

Benki ya Dunia inasema imetilia mkazo kuhusu utawala bora na udhibiti mkali kuhusu matumizi ya "pesa zetu." Mataifa ya Sahel yanazongwa na masuala ya usimamizi mbaya na rushwa miongoni mwa matatizo mengine. "Hii inamaana, ikiwa kuna rushwa na tukagundua, tutawashughulikia wale wanaotumia vibaya pesa zetu."

Chanzo: DW