1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa maandamano watishia kutolitii jeshi nchini Sudan

9 Mei 2019

Viongozi wa waandamanaji nchini Sudan wametishia kuanzisha kampeni kubwa ya nchi nzima ya kuwataka raia kutozitii mamlaka baada ya kuwatuhumu viongozi wa kijeshi kwa kukawia kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

https://p.dw.com/p/3IDrM
Afrika | Protests im Sudan
Picha: picture-alliance/dpa/AA/M. Hjaj

Maelfu ya watu bado wamepiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum kwa karibu wiki ya nne sasa baada ya vikosi vya jeshi kumtimua madarakani kiongozi mkandamizaji Omar al-Bashir kufuatia miezi kadhaa ya maandamano makubwa dhidi ya utawala wake.

Pande mbili zinazozana juu ya ikiwa baraza jipya la uongozi litalokabidhiwa madaraka ya mpito kutoka kwa baraza la kijeshi la sasa lenye majenerali pekee liwe na uwakilishi mkubwa wa raia au wanajeshi.

Wiki iliyopita muungano wa makundi ya waandamanaji, AFC, uliwasilisha mapendekezo yake juu ya muundo wa utawala wa kiraia ukijumuisha tawi la utawala na baraza la kutunga sheria ambavyo vitaiongoza nchi hiyo baada ya kuwaondoa majenerali wa jeshi.

Baraza la Mpito la Kijeshi lenye wajumbe kumi lilisema mnamo siku ya Jumanne kuwa limekubaliana na mapendekezo hayo lakini kuna masuala mengi yenye mashaka.

Jeshi linachelewesha kukabidhi madaraka

Sudan | Protest | Militär in Khartoum
Picha: Reuters/U. Bektas

Hapo jana (Mei 8) viongozi wa maandamano ya umma walisema Baraza la Kijeshi linachelewesha mchakato mzima wa kukabidhi madaraka.

Kiongozi wa waandamanaji, Khalid Omar, aliwaambia waandishi habari kuwa majibu ya baraza la kijeshi kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na muungano wa AFC yanavunja moyo na yanaiweka nchi hiyo kwenye hatari kubwa.

Kuhusu hatua wanazolenga kuchukua baada ya jeshi kueleza kuwa na masuala kadhaa ya kufanyia kazi kwenye mapendekezo yao, Khalid alisema hatua zitahusu kuongeza shinikizo dhidi yao na kuongeza kuwa "iwapo wataendelea kusalia madarakani na sisi tunawaandaa raia kutowatii".

Marekani yahimiza hatua za haraka

Naibu waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, John Sullivan, amemshinikiza kiongozi wa baraza la Jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kufikia makubaliano ya haraka na waandamanaji.

Kwenye mazungumzo kwa njia ya simu na Burhan mnamo siku ya Jumatano, Sullivan alitilia mkazo nia ya raia wa Sudan ya kuwa na hatma huru, yenye manufaa na ya kidemokrasia.

Sudan Khartum Demonstranten vor dem Militärhauptquartier
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Basheer

Sullivan alimuhimiza Burhan kuharakisha mchakato wa kuwezesha kuundwa kwa serikali ya mpito ya kirai na kufikia makubaliano na muungano wa AFC.

Muungano wa APC unaundwa na makundi ya siasa, viongozi na wanaharakati wengineo ambao wengi wanataka kuifanya Sudan kuwa taifa la lisilo la kidini.

Vyombo vya habari na tovuti nchini Sudan zimeripoti mara kadhaa kwamba viongozi wa maandamano wanataka suala la kuwa na dola inayozingatia sheria za kidini lijadiliwe baada ya kuundwa kwa utawala wa kiraia.

Mwadishi: Rashid Chilumba/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef