Viongozi wa maandamano Sudan waitisha tena maandamano
1 Mei 2019Wito huo unakuja wakati hali ya wasi wasi ikiongezeka kuhusiana na muundo wa baraza jipya la pamoja kati ya raia na jeshi litakaloiongoza nchi ya Sudan, wakati waandamanaji wakiimarisha vizuwizi nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum. Pande hizo mbili zina mambo mengi yanayokinzana kuhusiana na wawakilishi katika baraza hilo jipya ambalo linatarjiwa kuchukua nafasi ya baraza la kijeshi ambalo lilichukua madaraka baada ya kuondolewa madarakani Omar al-Bashir Aprili 11 baada ya maandamano makubwa ya umma kupinga utawala wake wa miongo mitatu.
Jeshi limekuwa likitaka baraza lenye wajumbe 10 ikiwa ni pamoja na wawakilishi saba wa jeshi na raia watatu.
Kutokubaliana kumesababisha Muungano kwa ajili ya Uhuru na mabadiliko kutangaza "maandamano ya watu milioni moja hapo Mei 2 , siku ya Alhamis kusisitiza dai lao kuu, ambalo ni utawala wa kiraia".
"Baraza la kijeshi halina nia thabiti juu ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa raia," amesema Mohamed Naji al-Assam , kiongozi wa chama cha wanataaluma wa Sudan SPA kilichoongoza maandamano.
"Baraza la kijeshi linasisitiza kwamba baraza la pamoja linapaswa kuongozwa na wanajeshi likiwa tu na wawakilishi wa kiraia," Assam amesema, na kuongeza kuwa jeshi limekuwa likitaka "kupanua madaraka yake kila siku".
"Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuunga mkono uchaguzi wa watu wa Sudan." Mohammed al-Asam alisisitiza:
"Tunahisi kutokana na vitendo vyote vya baraza la kijeshi la mpito hadi wakati huu kwamba halina nia ya dhati kuhamisha madaraka kwa raia, licha ya uthibitisho wa baraza hilo wakati lilipoingia madarakani, likithibitisha kwamba limeingia madarakani kutokana na madai ya umma na kuthibitisha kwamba litahamisha mamlaka kwa raia haraka iwezekanavyo. Sasa tunaona muda umepita wakati madaraka ya baraza la kijeshi yanaongezeka na hii ni hatari kwa mapinduzi ya Sudan."
Akizungumza katika mkutano huo huo na waandishi habari , Madani Abbas Madani , kiongozi mwingine wa maandamano, amelishutumu baraza la kijeshi kwa kutumia "lugha ya kuongeza mivutano ambayo haishawishi ushirikiano".
Taarifa zao zimekuja baada ya jenerali mwandamizi wa jeshi la Sudan kutangaza chombo hicho kipya kwamba kitaongozwa na kiongozi wa sasa wa kijeshi jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Waandamanaji wameliita baraza la kijeshi linaloongozwa na Burhan "kuwa ni nakala ya utawala ulioangushwa".
Wanataka wingi wa raia katika baraza litakalokuwa na wajumbe 15 pamoja na wanajeshi ambapo kutakuwa na wawakilishi saba kutoka jeshini.
Katika mfarakano unaoongezeka , baraza la kijeshi limesema wanajeshi sita wameuwawa katika makabiliano na waandamanaji nchi nzima siku ya Jumatatu.