1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Viongozi 11 wa nchi za Balkan waiunga mkono Ukraine

22 Agosti 2023

Viongozi wa nchi 11 za Balkan na Ulaya ya Mashariki wametia saini tamko la pamoja kuunga mkono uadilifu wa Ukraine katika mkutano mjini Athens. Tamko hilo liltiwa saini mbele ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky

https://p.dw.com/p/4VSDb
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis wapongezwa baada ya kutia saini makubaliano mjini Athens Ugiriki Jumatatu, Agosti 21, 2023
Maafisa wawapongeza rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis baada ya kutia saini makubaliano mjini Athens UgirikiPicha: Thanassis Stavrakis/AP/picture alliance

Hati hiyo ya kuunga mkono uadilifu wa Ukraine ilitiwa saini na viongozi kutoka Serbia, Moldova, Montenegro, Romania, Kosovo, Bosnia na Herzegovina, Macedonia ya Kaskazini, Bulgaria na Croatia, pamoja na Ugiriki iliyoandaa hafla hiyo. Rais wa baraza kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel na rais wa halmashuri kuu ya Umoja huo Ursula von der Leyen pia walihudhuria kongamano hilo.

Viongozi hao pia walielezea uungaji mkono na shukran zao kwa juhudi za Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika kuweka kanuni za amani kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Soma pia: Jeshi la Ukraine lavuka na kuingia katika jimbo la Kherson

Marubani wa Ukraine wa ndege za kivita chapa F-16 kupata mafunzo

Ugiriki ilikuwa imesema kuwa itasaidia kuwapa mafunzo marubani wa Ukraine wa ndege za kivita chapa F-16 na kusaidia katika ujenzi mpya wa Odesa. Siku ya Ijumaa, Ukraine ilipongeza uamuzi wa Marekani wa kuiruhusu Denmark na Uholanzi kupeleka ndege hizo za kivita chapa F-16 nchini Ukraine pindi marubani wake watakapopata mafunzo ya kuzitumia. Waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleskii Reznikov amesema ana imani kuwa mataifa zaidi hivi karibuni yatajiunga na kile kinachojulikana kama muungano wa anga kwa kutoa ndege zaidi za kivita chapa F-16 kwa Ukraine.

Ndege ya jeshi la wanahewa la Romania F16 iliopewa kikosi cha 53 cha wapiganaji "Warhawks"  yashika doria kwenye ukingo wa Mashariki wa NATO
Ndege ya jeshi la wanahewa la Romania F16 yashika doria kwenye ukingo wa Mashariki wa NATOPicha: Gianluca Vannicelli/IPA/picture alliance

Soma pia: Ugiriki kuwafunza marubani wa Ukraine kurusha ndege za F-16

Urusi yadai kuzuia uvamizi wa Ukraine

Katika hatua nyingine, gavana wa eneo la Bryansk nchini Urusi  Alexander Bogomaz amesema kuwa vikosi vya nchi hiyo vimezuia jaribio la wavamizi wa Ukraine la kuingia katika eneo hilo la Bryansk. Katika ujumbe kupitia mitandao ya kijamii, Bogomaz amesema kuwa wavimizi hao walijaribu kuingia kupitia mpaka wa wilaya ya Klimovsky.

Tazama pia:

NATO yajadili jinsi ya kuipatia Ukraine silaha zaidi

Ameongeza kuwa shambulizi hilo lilizuiwa na taasisi mbali mbali za usalama ikiwemo wizara ya Ulinzi, ulinzi wa kitaifa na FSB lakini hatua zinachukuliwa kuhakikisha usalama wa raia. Hata hivyo Ukraine imekanusha kuhusika na mashambulizi hayo na badala yake kuyalaumu makundi ya Urusi yanayompinga rais Vladimir Putin.

Mahakama ya ICC kusikiza pingamizi ya Urusi kuhusu kesi ya mauaji ya kimbari

Mahakama ya Kimataifa ya Haki -ICJ- imesema kuwa itasikiza pingamizi za Urusi kuhusu mamlaka yake katika kesi ya mauaji ya kimbari iliyowasilishwa na Ukraine, katika vikao vitakavyoanza Septemba 18. Ukraine iliwasilisha kesi hiyo muda mfupi baada ya uvamizi wa Urusi kuanza mnamo Februari 24,2022 ambapo iliishtumu Urusi kwa kutumia kwa uongo sheria ya mauaji ya kimbari kuhalalisha shambulizi hilo.