Vikao vya kusikiliza unyama wa Jammeh vyatimiza mwaka | Matukio ya Afrika | DW | 11.12.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Vikao vya kusikiliza unyama wa Jammeh vyatimiza mwaka

Raia wa Gambia wamefuatilia kwa karibu wakati ambapo mashahidi kadhaa wamemshutumu rais wao wa zamani Yahya Jammeh kwa ukatili katika vikao ambavyo vimekuwa na athari ndogo mno kwa wafuasi wake sugu.

Mwaka wa kwanza wa kusikilizwa kwa simulizi hizo uliisha wiki iliyopita na kutilia kikomo miezi kadhaa ambapo watu wamekuwa wakitoa ushahidi kuhusu mateso, mauaji na ubakaji ambao walipitia chini ya kiongozi huyo.

Dikteta huyo Yahya Jammeh aliiongoza nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi kwa miaka ishirini na miwili kabla ya kutoroka Januari mwaka 2017 baada ya kupoteza uchaguzi kwa Adama Barrow. Mashahidi 190 wamefika mbele ya Tume ya Ukweli na Maridhiano TRRC iliyobuniwa ili kuchunguza unyama uliofanywa katika mpango ulioanza mwezi Januari.

Tume itaandika ripoti baada ya vikao kukamilika mwaka ujao

Vikao vya tume hiyo ya maridhiano vinatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka miwili ingawa bado haijulikani iwapo vikao hivyo vitapelekea jammeh kufunguliwa mashtaka. Wakili mmoja wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch Reed Brody amesema vikao hivyo ni vya kubaini iwapo kuna kesi dhidi ya dikteta huyo.

Gambia Flüchtlinge | Rückkehrer an der Küste Banjuls

Gambia ni njia ya wahamiaji wanaoelekea Ulaya

Brody amesema tume hiyo itaandika ripoti mwishoni mwa vikao hivyo mwaka ujao ambapo inaaminika wataomba kurejeshwa kwa Jammeh nchini Gambia kutoka Guinea ya Ikweta.

Wanachama wa zamani wa kikosi cha mauaji cha rais huyo wa zamani wamemtuhumu kwa kuamrisha mauaji chungunzima. Kikosi hicho kiliwauwa wahamiaji hamsini wa Kiafrika ambao walifikiri ni wanamgambo, ambapo waliwauwa ufukweni wakati walipokuwa wanajaribu kuelekea Ulaya.

Mwezi Oktoba mwanadada mmoja aliyeshiriki mashindano ya urembo nchini Gambia alisema Jammeh alimbaka baada ya kukataa kuolewa naye.

Jammeh bado anaungwa mkono na wengi nchini Gambia

Vikao vya tume hiyo mwaka ujao bado vinatazamiwa kuendelea kuchunguza unyama wa utawala wa Jammeh kama kuwalazimisha wagonjwa walio na ukimwi kutumia dawa za miti shamba zilizovumbuliwa na yeye kama rais wakai huo.

Gambia Ex Präsident Yahya Jammeh

Yahya Jammeh yuko uhamishoni Guinea ya Ikweta

Licha ya yote haya, rais huyo wa zamani bado anaungwa mkono na wengi katika nchi hiyo yenye idadi jumla ya watu milioni mbili. Yankuba Colley ni mwanachama wa zamani wa chama tawala cha zamani na anasema kamba tume hiyo ni mbinu ya unafiki tu na wala haitoleta maridhiano nchini humo. Anadai kwamba wakili anayeendesha vikao hivyo hataki kusikia chochote isipokuwa kwamba Jammeh ndiye aliyehusika na unyama uliofanyika wakati huo.

Maelfu ya wafuasi wa chama cha Jammeh cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction APRC waliandamana katika mitaa ya mji mkuu Banjul mwezi uliopita wakitaka arudi nyumbani kutok uhamishoni.

Rais huyo wa zamani wa Gambia hajasikika tangu aende uhamishoni huko Guinea ya Ikweta mwaka 2017.