1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno yaelekea kwenye mkwamo wa kisiasa

Bruce Amani
11 Machi 2024

Ureno inakabiliwa na kipindi cha mkwamo wa kisiasa kufuatia uchaguzi wa bunge ambao hakuna chama kilichopata ushindi wa moja kwa moja wa wingi wa viti kuweza kuunda serikali katika taifa hilo la Ulaya.

https://p.dw.com/p/4dOlz
Luis Montenegro
Luis Montenegro, kiongozi wa chama cha Democratic Alliance kilichopata viti vingi kwenye uchaguzi wa bunge nchini Ureno, lakini ambavyo havitoshi kuunda serikali.Picha: MIGUEL RIOPA/AFP/Getty Images

Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia, Democratic Alliance, ambacho kilishinda wingi wa viti katika uchaguzi huo wa siku ya Jumapili (Machi 10), kilitarajiwa kuombwa kujaribu kuunda serikali.

Lakini japokuwa chama hicho kilikipiku kile kilichoko madarakani cha Kisoshalisti lakini kilipata tu viti 79, idadi ambayo haifiki wingi unaohitajika katika bunge lenye viti 230.

Soma zaidi: Wasoshalisti waondolewa madarakani Ureno

Democratic Alliance ilihitaji uungwaji mkono wa chama cha siasa za mrengo wa kulia kinachopinga sera za uhamiaji cha Chega ili kupata idadi ya viti 116 katika bunge la Lisbon.

Chega kilipata viti 48 kutoka 12 ilivyopata katika uchaguzi wa 2022.