1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani kuitisha maandamano tarehe 3.

1 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CieI

Nairobi.

Zaidi ya watu 100 wanasemekana kuwa wameuwawa katika ghasia ambazo zimezuka nchini Kenya kufuatia kuchaguliwa tena kwa rais Mwai Kibaki siku ya Jumapili. Matangazo kwa njia ya televisheni yamesitishwa na maafisa wa serikali ya Kenya wakati polisi walitumia mabomba ya maji, mabomu ya kutoa machozi na risasi kuzima ghasia hizo.

Akizungumzia ghasia hizo mgombea wa upinzani Raila Odinga ameilaumu serikali kwa kusababisha wananchi kufanya ghasia kupitia majeshi ya usalama.

Idadi ya matukio tuliyoyapata sio kutoka kwa watu, lakini serikali kupitia majeshi yake ya usalama yanajaribu kuwakorofisha watu, na wanawapiga risasi. Na kwa hiyo tutaitisha maandamano makubwa nchi nzima, maandamano ya amani kabisa.

Amri ya kutotembea ovyo mchana imewekwa katika mji wa Kisumu, na polisi katika mji huo wamepewa amri ya kumpiga mtu yeyote risasi ambaye atakwenda kinyume na amri hiyo. Mgombea wa upinzani Raila Odinga ambaye alikuwa mbele katika maoni ya wapiga kura kabla ya uchaguzi amesema kuwa rais Kibaki amefanya njama ya wizi wa kura. Umoja wa Ulaya na wachunguzi wengine katika uchaguzi huo wameeleza kutoridhishwa kwao kwa kiasi kikubwa kuhusiana uhalali wa matokeo ya uchaguzi huo.