1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upande wa upinzani washinda Georgia

2 Oktoba 2012

Muungano wa vyama vya upinzani unaoongozwa unaonyesha kukipita chama tawala katika uchaguzi wa bunge ulioitishwa jana nchini Georgia. Hayo ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa hadi sasa.

https://p.dw.com/p/16Ieg
Wageorgia washerehekea ushindi mjini TiblisiPicha: DW/Amalia Oganjanyan

Chama cha "Ndoto ya Georgia" kinachoongozwa na mfanyabiashara bilioneya Bidzina Ivanishvili kimejikingia asilimia 53 ya kura hadi sasa huku chama tawala cha "Vuguvugu la taifa" kikijikusanyia asili mia 41, baada ya asili mia 20 ya kura kuhesabiwa hadi sasa.

"Yadhihirika kana kwamba tutakuwa na bunge jengine kabisa" amesema Ivanishvili kupitia televisheni ya upande wa upinzani, leo asubuhi na kuongeza: "Kwa mara ya kwanza katika historia ya Georgia,wananchi wanaweza kusababisha mabadiliko ya serikali kupitia uchaguzi.Tunabidi tuwe macho,yote yaliyopita tuyasahau na tuijenge Georgia mpya.Viti visivyopungua 100 vya bunge tunavimiliki sisi."

Rais Mikheil Saakashvili ameonya dhidi ya pupa. Ingawa amekiri kwamba chama chake kimeshindwa katika mji mkuu Tblisi, hata hivyo anasema Georgia ina majimbo mengine pia. Rais Saakashvili ametoa mwito watu wasubiri hadi matokeo ya mwisho yatakapotangazwa.Msemaji wa kampeni ya uchaguzi ya chama tawala amesema kwa upande wake kutokana na mfumo wa upigaji kura nchini Georgia, chama cha Vuguvugu la taifa kinaweza kujikingia viti vingi zaidi vya moja kwa moja.

Georgien Parlamentswahl 2012 Tbilisi Mikhail Saakashvili
Rais anaemaliza wadhifa wake Mikhail SaakashviliPicha: dapd

Bila ya hata kusibiri matokeo rasmi kutangazwa,wafuasi wa upande wa upinzani waliokusanyika katika uwanja wa uhuru walihanikizi kwa furaha na kushangiria:

Hakuna vurugu zozote zilizoripotiwa katika jamhuri hiyo ya zamani ya usovieti yenye wakaazi milioni nne na laki tano.

Jumuia ya usalama na ushirikiano barani Ulaya inatarajiwa kutangaza ripoti yake baadae hii leo kuhusu jinsi uchaguzi huo ulivyopita.

Katika uchaguzi uliopita wa bunge,mwaka 2008,chama cha Vuguvugu la taifa cha rais Mikheil Saakashvili kilijipatia viti 119 kati ya 150.

Georgien Parlamentswahl 2012 Tbilisi Bidzina Ivanishvili
Kiongozi wa upande wa upinzani Bidzina IvanishviliPicha: dapd

Uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu kwa rais huyo aliyesomea Ufaransa na Marekani na ambae kuingia kwake madarakani kufuatia mapinduzi ya mawardi,kuliielekeza nchi hiyo upande wa magharibi na kuiudhi Urusi.

Mageuzi ya katiba yatalipatia bunge na waziri mkuu madaraka makubwa zaidi kuanzia mwaka 2013-mwaka utakaohitimisha awamu ya pili na ya mwisho ya utawala wa Saakashvili.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef