Umoja wa Ulaya kutoa dozi milioni 1 za chanjo dhidi ya virusi vya Corona kwa nchi masikini | NRS-Import | DW | 21.05.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Janga la Corona lawakusanya wakuu wa dunia

Umoja wa Ulaya kutoa dozi milioni 1 za chanjo dhidi ya virusi vya Corona kwa nchi masikini

Viongozi wa nchi na serikali na mashirika 12 ya kimataifa wakutana kwa njia ya mtandao katika mkutano mkuu wa kilele kuhusu hali ya afya duniani

Umoja wa Ulaya umeahidi kuchangia dozi milioni 100 za virusi virusi vya Corona kwa nchi masikini.Ahadi ya Umoja huo imetolewa leo Ijumaa wakati ukifunguliwa mkutano wa kilele wa dunia kuhusu namna ya kujikwamua na janga hilo na kuepusha janga jipya.

Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ametangaza hatua ya Umoja huo ya kuchangia chanjo katika nchi masikini, akiwa sambamba na waziri mkuu wa Italia Mario Draghi ambaye nchi yake inashikilia kwa sasa nafasi ya mwenyekiti wa kundi la nchi tajiri za G20 na ndiyo muandaaji mwenza wa mkutano huo wa kilele.  Von der Leyen amesema Umoja wa Ulaya utatangaza juhudi mpya za kuunga mkono utengenezaji chanjo katika bara la Afrika kwasababu wanaamini chanjo zinapaswa kuwafikia watu wote kila mahala.Na juu ya hilo akasema.

"Timu Ulaya inalenga kuchangia kiasi dozi milioni 100 katika nchi za kipato cha chini na  wastani  kufikia mwishoni mwa mwaka 2021.''

Viongozi wa dunia wanatarajiwa kutumia mkutano huu wa kilele kusisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za kutoa chanjo kote ulimwenguni kupitia michango,kuimarisha utengenezaji wa chanjo hizo pamoja na kuepuka hatua za kuzuia usafirishwaji nje chanjo hizo.Waziri mkuu wa Italia Mario Draghi kwa upande wake amehimiza juu ya ulimwengu kujitajidi kuzuia janga jingine la virusi vya Corona.

''Tunapojiandaa kwa janga jingine,kipaumbele chetu kinapaswa kuhakikisha kwamba sote tunalishinda janga la sasa kwa pamoja.Tunapaswa kuuchanja ulimwengu na tunapaswa kufanya hivyo haraka.''

Hata hivyo azimio la mwisho la mkutano huo wa kilele wa dunia halitarajiwi kuidhinisha fikra inayokabiliwa na utata ya kuruhusu utolewaji kibali cha muda duniani cha kuwapa haki miliki wataalamu wanaogundua chanjo ya virusi vya Corona.

Badala yake viongozi watapigia upatu matumizi ya njia nyingine kama vile kuruhusu kuwepo kibali cha makubaliano ya hiyari ya ubadilishanaji wa teknolojia. India na Afrika Kusini kwa miezi sasa zimekuwa zikiongoza miito ya kutaka ichukuliwe hatua ya kuondolewa kwa muda sheria za kulinda haki miliki ya ugunduzi wa kitaalamu kuhusiana na suala la chanjo ili kuimarisha utengenezwaji wa chanjo hizo,hatua ambayo hivi karibuni iliungwa mkono na Marekani lakini ikitiliwa mashaka sana na Umoja wa Ulaya.

Ripoti moja iliyotolewa na taasisi yenye ushawishi mkubwa duniani ilionya mwanzoni mwanzoni mwa mwezi huu kwamba kiwango cha janga la Covid 19,ambalo limeua zaidi ya milioni 3.4 duniani kingeweza kuzuilika.Jopo huru la taasisi ya kukabiliana mapema na majanga ilisema mchanganyiko hatari wa malumbano na ushirikiano dhaifu ndiyo yaliyosababisha tahadhari zilizotolewa mwanzo kupuuzwa.

Kiasi viongozi 20 wakuu wa nchi na serikali na mashirika 12 ya kimataifa ikiwemo shirika la afya duniani WHO,Umoja wa Afrika,shirika la biashara duniani WTO na benki ya dunia wanashiriki mkutano huo wa kilele kwa njia ya mtandao.

Mwandishi:Saumu Mwasimba