1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika waisimamisha Burkina Faso baada ya mapinduzi

Iddi Ssessanga
31 Januari 2022

Umoja wa Afrika umesema Jumatatu kuwa umeisimamisha Burkina Faso uanachama kufuatia mapinduzi ya Januari 24 yaliomuondoa madarakani rais Roch Marc Christian Kabore.

https://p.dw.com/p/46Jpe
Burkina Faso | Neue Militärjunta
Picha: Olympia de Maismont/AFP

Baraza la Amani na Usalama la umoja huo lenye wajumbe 15, lilisema kupitia mtandao wa kijamii wa twitter kwamba "lilipiga kura kusitisha ushiriki wa #BurkinaFaso katika shughuli zote za Umoja wa Afrika hadi itakaporejesha kikamilifu utaratibu wa kikatiba nchini humo."

"Baraza laamua kufuatana na utaratibu unaohusika..kusimamisha ushiriki wa Burkina Faso katika shuguli zote za Umoja wa Afrika hadi utaratibu wa kikatiba utakaporejeshwa kikamilifu nchini humo," ilisema idara ya masuala ya kisiasa, amani na usalama ya Umoja wa Afrika katika ujumbe huo wa twitter.

Soma pia: Jeshi laahidi kurejesha usalama Burkina Faso

Tayari Moussa Faki Mahamat, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, alikuwa amelaani mapinduzi kabla ya utawala kijeshi kutangaza rasmi kwamba ulikuwa umemuondoa rais Roch Marc Kabore.

Mapinduzi ya Burkina Faso ndiyo ya duru ya karibuni zaidi ya machafuko kulikumba taifa hilo maskini na lisilo na bandari, ambalo limekabiliwa na hali tete na ukosefu wa utulivu tangu kupata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.

Burkina Faso Anhänger feiern Militärputsch
Waandamanaji mjini Ouagadougou wakionesha kuunga mkono utawala wa kijeshi wakiwa na picha ya Kanali Assimi Goita wa Mali na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba wa Burkina Faso, Januari 25, 2022.Picha: OLYMPIA DE MAISMONT/AFP

Kiongozi wa mapindizi hayo, Luteni Kanali Paul-Henri Damiba, hajatangaza mpango wa Burkina Faso kurejea kwenye utawala wa kikatiba mbali ya ahadi isiyo wazi ya kufanya hivyo "wakati mazingira yatakapokuwa sawa."

Tayari nchi hiyo imesimamishwa kutoka jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya kanda ya Afrika Magharibi, ingawa ECOWAS imesita kuiwekea vikwazo baada ya mapinduzi hayo ya Januari 24.

Ujumbe wa ECOWAS pamoja na mjumbe wa Umoja wa Mataifa walitarajiwa kuitembelea Burkina Faso siku ya Jumatatu ili kukutana na viongozi wa mapinduzi kabla ya kuamua juu ya hatua zinazofuata.

Soma pia: Jeshi Burkina Faso lakemewa licha ya uungwaji mkono

Umoja wa Afrika ulisitisha wanachama wengine wawili wa Afrika Magharibi,Mali na Guinea, baada ya majeshi yake kuchukuwa madaraka mwaka jana kwa njia ya mapinduzi. Mapinduzi ya Burkina Faso yalikuwa ya nne katika kanda hiyo katika muda wa miezi 18.

ECOWAS na washirika wake wamelaani mapinduzi, ambayo wanahofia yanaweza kuvuruga zaidi taifa hilo linalokumbwa tayari na vurugu za wapiganaji wa itikadi kali, lakini wanajikutana wakiwa na ushawishi mdogo.

Kiongozi wa mapinduzi ya Burkina Faso, Luteni Kanali Paul-Henri Damiba, alisema wiki iliyopita kwamba nchi hiyo itarejea kwenye utawala wa kikatiba pale "mazingira sahihi yatakapokuwepo."

Ghana Accra | Economic Community of West African States | ECOWAS
Viongozi wa ECOWAS wamesimamisha uanachama wa Burkina Faso lakini wamesita kuiwekea vikwazo hadi wakutane na utawala mpya.Picha: IVORY COAST PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Ukosefu wa usalama na mapinduzi

Uasi wa wapiganaji wa itikadi kali ambao umesambaa nje ya mipaka ya Mali umesababisha vifo vya watu zaidi ya 2,000 na kuwalaazimu milioni 1.5 kukimbia makaazi yao tangu 2015. Kati ya 2015 na 2018, mashambulizi ya kigaidi yameulenga mji mkuu Ouagadougou na maeneo mengine muhimu.

Tangu 2019, mashambulizi ya vikosi vinavyohama vya mapambano yamelenga hasa maeneo ya vijijini kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo, na kuchochea ukosefu mkubwa wa makaazi na vurugu za kijamii.

Soma pia: Burkina Faso kukabiliwa na hali tete zaidi?

Watu wapatao 2,000 waliuawa, miongoni mwao wakiwemo raia na wanachama wa vikosi vya kijeshi au wapiganaji wa kundi la kujitolea la "Volunteers for the Defence of the Homeland", ambalo ni kundi la ulinzi wa kiraia lililoundwa mwaka 2020.

Wapiganaji wa Kiislamu hivi sasa wanatembea kwa uhuru zaidi katika maeneo makubwa ya nchi na wamewalaazimu wakaaz wa baadhi ya maeneo kutii tafsiri yao kali ya shariah. Wakati huo huo, mapambano yanayoendelea ya jeshi dhidi ya wapiganaji hao yamekomba rasilimali zote chache za taifa hilo.

Infografik Putsche in ECOWAS Staaten seit 2020 DE
Ramani inayoonyesha mataifa matatu ya Afrika Magharibi yanayotaliwa na wanajeshi baada ya kuzipindiua serikali za kiraia.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa kilele wa wakuu wa matifa jumuiya ya ECOWAS siku ya Ijumaa, rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, ambaye ni kaimu mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alisema ECOWAS ina kazi kubwa ya kufanya kuwashawishi watu kuhusu faida za demokrasia.

Chanzo: Mashirika