1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu washindwa kuwalinda raia kwenye maeneo ya mizozo

Grace Kabogo
24 Mei 2023

Antonio Guterres: Ulimwengu umeshindwa kuwalinda raia, wanaonaswa katika mizozo.

https://p.dw.com/p/4RkHp
UN Generalsekretär Antonio Guterres / New York
Picha: Fatih Aktas/AA/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema ulimwengu umeshindwa kuwalinda raia, huku idadi ya watu walionaswa katika mizozo ikiongezeka mwaka uliopita.

Mwaka 2022 Umoja wa Mataifa ulirekodi asilimia 53 ya ongezeko la vifo vya raia, ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, huku takribani vifo vya raia 17,000 vikirekodiwa kwenye mizozo 12.

Akitolea mfano vifo vya raia nchini Ukraine na Sudan, shule zilizoharibiwa Ethiopia na uharibifu wa miundombinu ya maji Syria, Guterres jana alilionya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ulimwengu umeshindwa kutimiza ahadi yake ya kuwalinda raia, ambayo iliwekwa katika sheria ya kimataifa ya kiutu.

Guterres amesema ulimwenguni kote, idadi ya wakimbizi waliolazimishwa kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita, mizozo, ukiukaji wa haki za binaadamu na mateso, imefikia milioni 100.