1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wa Kiislam washeherekea Eid al-Fitr

25 Juni 2017

Waislamu nchini Saudi Arabia na takriban katika nchi nyengine 14 Jumapili (25.06.2017) wanasheherekea siku ya kwanza ya sherehe za Eid al-Fitr ambazo zinaadhimisha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa mfungo wa Ramadhan.

https://p.dw.com/p/2fLMK
Saudi Arabien Medina nach Selbsmord-Attentat nahe der  Prophetenmoschee 2016
Picha: Getty Images/AFP

Saudi Arabia ambayo ni maskani ya maeneo takatifu kabisa ya Waislamu imetangaza hapo Jumamosi kwamba ilikuwa ndio siku ya mwisho ya Ramadhan.Matangazo kama hayo pia yametolewa Misri,Umoja wa Falme za Kiarabu,Bahrain, Qatar,Jordan,Kuwait,Libya,Palestina,Syria  Sudan na Yemen.

Indonesia nchi ambayo ina idadi kubwa kabisa ya Waislamu duniani halikadhalika Malaysia pia zimesheherekea Eid Jumapili.Hata hivyo Oman itasheherekea siku ya kwanza ya Eid al -Fitr hapo Jumatatu(26.06.2017) kwa mujibu wa shirika la habari la serikali nchini humo.

Rais Bashar al Assad wa Syria ameongoza sala ya Eid katika mji wa kati wa Hama na kujitokeza hadharani nje ya mji mkuu wa nchi hiyo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwaka mmoja.

Ofisi ya Assad imechapisha picha zikimuonyesha akisali ndani ya msikiti wa Al-Nuri uliokuwa ukimeremeta mataa wakati wa alfajiri kabla ya kuwaumini waliokuwa nje.

Kabla ya sherehe hizo serikali ya Syria imewaachilia huru zaidi watu 670 waliokuwa wakishikiliwa wakiwemo baadhi ya watoto waliokuwa wamezaliwa na wafungwa kutoka magerezani karibu na mji mkuu wa Damascus.

Mara ya mwisho Assad kuonekana hadharani ilikuwa ni mwezi wa Julai mwaka 2016 wakati wa sherehe za Eid-al-Fitr katika mji wa tatu kwa ukubwa nchini humo wa Homs.

Asia waiombea amani

Syrien Bashar al-Assad beim Gebet in einer Moschee in Hama
Rais Bashar al Assad katika sala ya Eid al-Fitr .Picha: Reuters/Sana

Waislamu barani Asia wamesheherekea Eid al-Fitr kwa sala kuiombea amani.Katika mji mkuu wa Indonesia Jakarta waumini wamesema wanataraji moyo wa Eid utazishinda hofu juu ya kuongezeka kwa harakati za wanamgambo katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya Waisamu duniani.

Nchini Malaysia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen vilikuwa mawazoni mwa baadhi ya waumini katika mji mkuu wa Kuala Lumpur.

Nchini Pakistan sherehe hizo zimeingia kiwingu baada ya takriban watu 150 kuuwawa katika mkasa wa moto uliozuka nchini  baada ya lori la kubeba mafuta kupinduka na watu kulikimbilia ili kuchota mafuta kabla ya kushika moto.

Eid al-Fitr inaadhimisha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo Waislamu walikuwa wakifunga kuanzia jua linapozama wakati wa alfajiri hadi linapotua wakati wa magharibi.

Eid al Fitr hutegemea kuonekana kwa mwezi na sherehe zake hupishana na kutofautiana baina ya nchi na nchi.Siku huanza kwa sala za asubuhi na mapema na baadae familia hutembeleana na kula vyakula maalum pamoja vile vya tamu tamu.

Wakati wa sherehe hizo za siku tatu watoto huvaa nguo mpya na hupatiwa zawadi za fedha raslim.Nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania na Kenya zitasheherekea Eid hapo Jumatatu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri :Caro Robi