1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukeketaji wapungua miongoni mwa wasichana wadogo

Sylvia Mwehozi
7 Novemba 2018

Timu ya wataalamu kutoka Uingereza na Afrika Kusini, imechapisha ripoti ya utafiti ambao imeufanya kwa miongo kadhaa, ambayo inaonyesha kupungua kwa visa vya ukeketaji kwa wasichana walio na umri chini ya miaka 14.

https://p.dw.com/p/37ngL
Sudan - Mädchen - Kinderheirat
Picha: picture-alliance/OKAPIA KG/W. Dolder

Timu ya wanasayansi iliyochapisha ripoti hiyo inasema imefanya uchunguzi wa kisasa wa takwimu za ukeketaji, ikizimulika jumla ya nchi 29, kuanzia miaka ya 90.

Kihistoria, viwango vya ukeketaji vimekuwa juu maeneo ya Afrika Mashariki. Mwaka 2016, kwa mfano shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto, lilisema kwamba asilimia 98 ya wanawake na wasichana nchini Somalia wamepitia ukeketaji.

Mila hiyo ya tangu jadi katika baadhi ya jamii  imekuwa ikipigiwa kelele na wanaharakati wa haki za wanawake na inaweza kusababisha matatizo ya kiafya na kisaikolojia, lakini bado imeendelea kutekelezwa pakubwa katika maeneo ya Afrika na Mashariki ya kati.

Matokeo ya utafiti wa timu hiyo ya wanasayansi kutoka Uingereza na Afrika Kusini yanaonyesha kwamba vitendo hivyo vimepungua hatua kwa hatua miongoni mwa watoto wadogo, ambao wako katika hatari kubwa.

Bildergalerie Afrika Genitalverstümmelung
Msichana wa Kipokot akiandaliwa kabla ya kukeketwaPicha: Reuters/S. Modola

Timu hiyo ya watafiti ilibaini kwamba vitendo vya ukeketaji katika eneo la Afrika Mashariki vimepungua kutoka asilimia 71 mwaka 1995 hadi asilimia 8 mwaka 2016. Profesa Ngianga-Bakwin Kandala kutoka chuo kikuu cha Northumbria nchini Uingereza, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba, "takwimu za sasa zinaonyesha kwamba zaidi ya wanawake na watoto milioni 200 duniani wamekeketwa".

Nchi za Afrika mashariki zenye idadi kubwa za Kenya na Tanzania, zenye viwango vya chini vya ukeketeji kati ya asilimia 3 hadi 10 vya wasichana kila mwaka, vilikuwa na mwelekeo wa kushuka katika ukeketaji.

Nchini Eritrea hata hivyo, wastani wa asilimia 67 ya wasichana wanalazimika kupitia mchakato wa ukeketaji kila mwaka kati ya mwaka 1995-2002.

Ripoti hiyo imepokelewa kwa mashaka na wanaharakati dhidi ya ukeketaji wa wanawake. Mmoja wa wanaharakati hao, jamillah Mwanjisi kutoka shirika la Save the Children nchini Somalia amesema ukeketaji bado ni tatizo kubwa. na kuongeza kuwa hakuna utashi wa kutosha kisiasa na kisheria kuufanya ukeketaji kuwa haramu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba