1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa ECOWAS: Kuna "matumaini" Mali

23 Agosti 2020

Ujumbe wa viongozi waandamizi wa Afrika Magharibi uliozuru Mali kwa ajili ya kuharakisha mchakato wa kurejea kwa utawala wa kiraia umesema una "matumaini" baada ya kukutana na jeshi lililomteka rais wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3hM9A
Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern | Goodluck Jonathan
Picha: Reuters/M. Kalapo

Mkuu wa Ujumbe huo wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, aliyekuwa rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amesema rais wa Mali aliyezuiliwa na wanajeshi hao Ibrahim Boubacar Keita anaendelea vyema.

"Tumemuona, yuko sawa kabisa," alisema Jonathan ambaye awali alikutana na wanajeshi waliochukua madaraka siku ya Jumanne. Wamekutana pia na kanali Assimi Goita ambaye ni mkuu wa jeshi hilo.

Mkuu wa kamisheni ya ECOWAS Jean-Claude Kassi Brou amesema mazungumzo hayo yalifanyika katika "mazingira ya uwazi na walihisi haja ya kuendelea mbele." Kassi Brou ameongeza kwamba wanatazamia kukamilisha kila kitu ifikiapo Jumatatu.

Ujumbe wa ECOWAS umetembelea kambi ya Kati

Ismael Wague ambaye ni msemaji wa jeshi lililo uongozini kwa sasa ambalo kwa sasa linajiita Kamati ya Kitaifa ya Ukombozi wa Watu, amesema pia kwamba mazungumzo yanaendelea vyema. "Tunaelewa kwamba marais kama Alassanne Ouattara wa Ivory Coast wanafanya juhudi za kupunguza mivutano kwa ajili ya suluhisho la amani hata ingawa wameshutumu unyakuaji wetu wa madaraka. Tunakaribisha mazungumzo," duru hiyo imeliambia shirika la habari la AFP.

Mali Proteste in Bamako
Malefu ya raia wa Mali wakisherehekea kuondolewa madarakani kwa Rais KeitaPicha: picture-alliance/AA/A. O. Toure

Ujumbe huo wa viongozi wa Afrika Magharibi pia umetembelea kambi ya jeshi ya Kati nje ya Mji Mkuu Bamako ambako mapinduzi hayo yalipoanzia. Rais Keita amekuwa akizuiliwa katika kambi hiyo pamoja na waziri mkuu Boubou Cisse na maafisa wengine waandamizi.

Maelfu ya raia wa Mali walijitokeza katika mitaa ya Bamako Ijumaa kusherehekea kuondolewa madarakani kwa Rais Keita aliyechaguliwa kwa mara nyengine mwaka 2018 ila baada ya muda mambo yakamgeukia na akaanza kukosolewa pakubwa.

"Nina furaha! Tumeshinda," alisema Mariam Cisse mwandamanaji mwenye umri wa miaka 38.

Ila mambo yalikuwa tofauti Jumamosi pale kundi moja la watu lilipojaribu kuandamana katika Mji Mkuu wa Bamako kwani walitawanywa na maafisa wa polisi.

"Tuko hapa leo kuonyesha kwamba hatukubaliani na mapinduzi haya ila watu walitushambulia kwa mawe kisha polisi wakawatawanya wafuasi wetu," alisema Abdoul Niang, mwanaharakati anayemuunga mkono rais Keita.

Rais Keita alitekwa na wanajeshi waasi Jumanne

Kumekuwa na shinikizo la kimataifa kutaka amani irejee nchini Mali huku Marekani hapo Ijumaa ikisimamisha msaada wa kijeshi kwa Mali ikisema hakutokuwa na mafunzo tena kwa wanajeshi wa nchi hiyo.

Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern | Assimi Goita
Kanali Assimi Goita mkuu wa jeshi lililochukua uongozi MaliPicha: Reuters/M. Kalapo

Kulingana na ratiba iliyoshuhudiwa na shirika la habari la AFP ujumbe wa ECOWAS utakutana na mabalozi wa nchi tano zenye viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani mapema Jumapili.

Wanajeshi waasi walimteka Rais Keita na viongozi wengine baada ya mapinduzi siku ya Jumanne, hilo likiwa ni pigo kubwa kwa nchi ambayo inakabiliana na ugaidi na kutoridhishwa pakubwa na serikali yake.

Mwaka 2013 Rais Boubacar Keita alishinda uchaguzi ambapo alijiwasilisha kama nguzo ya umoja katika nchi iliyogawika na akachaguliwa tena 2018 kwa muhula mwengine wa miaka mitano. Ila alishindwa kukabiliana na ugaidi ambao umepelekea baadhi ya maeneo ya nchi hiyo mikononi mwa wanamgambo wa Kiislamu na kuchochea machafuko ya kikabila.

Katika ishara ya changamoto hiyo ya usalama inayoikabili Mali, wanajeshi 4 waliuwawa Jumamosi kutokana na bomu lililokuwa limetegwa katikati mwa nchi hiyo.