Ujerumani yaikandamiza San Marino 8-0
12 Novemba 2016Serge Gnabry alipachika mabao matatu katika mchezo wake wa kwanza na timu ya taifa ya Ujerumani, Die Mannschaft, wakati mabingwa hao wa kombe la dunia wakiisambaratisha San Marino kwa mabao 8 bila majibu jana Ijumaa (11.11.2016) katika mchezo wa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Mlinzi wa kushoto Jonas Hektor aliongeza mabao mawili wakati kocha Joachim Loew alitimiza ushindi wa michezo 95 kama kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani , Die Mannschaft. Ushindi wa nne wa Ujerumani, ikifunga mabao 16 bila ya kufungwa bao, umeimarisha uongozi wake katika kundi C.
San Marino , taifa dogo sana linalozungukwa na Italia , haikufanikiwa kupiga mpira hata mara moja langoni mwa Ujerumani na inaendelea kubaki bila ushindi katika michezo 126.
Pamoja na hayo , San Marino imefanya vizuri kuliko miaka 10 iliyopita , wakati ilipokandikwa mabao 13-0 na Ujerumani katika mchezo wa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya.
Ikicheza bila ya wachezaji wake kadhaa wa timu ya kwanza katika uwanja ambapo mvua kubwa ilikuwa inanyesha , Loew aliteua wachezaji wawili wapya kwa ajili ya kuanza mchezo wa jana katika uwanja wa San Marino mjini Serravalle, na mmojawao alikuwa mlinzi Benjamin Henrichs, ambaye ndie alianza kuvurumusha mkwaju wa kwanza golini mwa San Marino, na kukosa kwa sentimita chache. Bao la kwanza lilifungwa na Sami Khedira , Gnabry akapachika mabao mengine mawili. Gnabry alifunga bao la nne muda mfupi baada ya kipindi cha pili, baada ya Hector kufunga bao la tatu.
Mabao mengine yalifungwa na Mattia Stefanelli alijifunga mwenyewe na kisha Kevin Volland alikamilisha karamu ya mabao kwa Ujerumani kwa kufunga bao la nane. Serge Gnabry , ambaye hivi sasa anachezea Werder Bremen anakuwa mchezaji wa pili kufunga mabao matatu katika siku ya kwanza kuchezea timu ya taifa tangu alipofanya hivyo Dieter Mueller zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Katika mchezo mwingine mjini Prague , Michael Krmencik alifunga bao katika mchezo wake wa kwanza na Jamhuri ya Cheki na Jaromir Zmrhal aliongeza bao la pili kwenye timu wenyeji, kabla ya Norway kupata bao la kufutia machozi la dakika za mwisho lililofungwa na Joshua King. Ulikuwa ushindi wa kwanza katika kundi C kwa Jamhuri ya Cheki , ambayo hivi sasa ina pointi tano na katika nafasi ya tano katika kundi hilo.
Ireland ya kaskazini ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Azerbaijan, na timu hiyo imesogea hadi nafasi ya tatu katika kundi C.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Sylvia Mwehozi