Uhalifu mpya wa kivita waripotiwa Sudan Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 19.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Uhalifu mpya wa kivita waripotiwa Sudan Kusini

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeituhumu serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi wanoegemea serikali kwa kufanya uhalifu wa kivita wakati wa operesheni mapema mwaka huu.

Ripoti mpya ya shirika la Amnesty International inasema unyama wa kutisha uliofanywa wakati wa harakati ya kijeshi nchini Sudan Kusini, yakiwamo mauaji ya raia, ubakaji wa wanawake na wasichana ulioratibiwa na wizi na uharibifu mkubwa wa mali, ulichochewa na maafisa wa serikali kushindwa kuwafungulia mashitaka au kuwatimua washukiwa wa uhalifu wa kivita.

Ripoti hiyo iliyopewa jina - "Kila kitu kilichokuwa kikipumua kiliuliwa: Uhalifu wa kivita katika kaunti za Leer na Mayendit, Sudan Kusini", imeandaliwa kutokana na ushuhuda uliotolewa na raia wapatao 100 ambao walifanikiwa kuikimbia operesheni ya majeshi ya serikali na makundi ya vijana waasi katika jimbo la kusini la Unity kati ya mwisho wa mwezi Aprili na mapema mwezi wa Julai mwaka huu.

Joan Mariner, Mshauri Mkuu anayehusika na masuala ya mizozo wa shirika la Amnesty International alisema sababu muhimu iliyochechoe operesheni hiyo ya kinyama ni kushindwa kuwashitaki washukiwa waliohusika na matukio ya awali ya machafuko yaliyowalenga raia katika eneo hilo. Mariner pia alisema kaunti za Leer na Mayendit zimeathiriwa zaidi miaka ya nyuma, lakini serikali ya Sudan Kusini inaendelea kuwapa washukiwa uhuru wa kufanya ukatili mpya. Matokeo yake yamegeuka kuwa janga kwa raia.

"Maafisa wa vikosi vya usalama vya serikali na waasi kwa makusudi waliwashambulia na kuwaua raia, wakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wanaoishi na ulemavu. Pia waliwateka nyara na kuwabaka wanawake na wasichana, kuwapeleka katika kambi zao za kijeshi, kuwabaka kwa makundi na kuwafanya watumwa wa ngono."

Raia waliuliwa vijijini

Ripoti ya Amnesty International ilisema jimbo la Unity lilikabiliwa na baadhi ya visa vibaya kabisa vya ukatili tangu mzozo wa Sudan Kusini ulipozuka miaka mitano iliyopita. Wimbi la hivi karibuni la machafuko liliibuka Aprili 21 mwaka huu na kuendelea hadi mapema mwezi wa Julai, wiki moja baada ya mkataba wa sasa wa amani, ambao ulisainiwa mnamo tarehe 27 mwezi Juni.

Südsudan Sudd Sumpfgebiete Nuer Stamm

Wanajeshi waliwasaka watu waliokimbilia maeneo ya chepechepe kama hili katika jimbo la Unity State

Wanaume na wanawake kadhaa waliliambia shirika la Amnesty International jinsi operesheni hiyo ilivyogubikwa na unyama usioelezeka, huku raia wakipigwa risasi kwa makusudi na kuuawa, kuchomwa wakiwa hai, kunyongwa juu ya miti na kukanyagwa na magari katika maeneo yanayodhibitiwa na upinzani katika kaunti za Mayendit na Leer. Wanajeshi na waasi wanaoegemea upande wa serikali walitumia magari kuwasaka raia waliokimbia kujificha katika maeneo ya chepechepe na kuwaua kwa kuwapiga risasi.

Mahakama ya uhalifu kuundwa

Joan Mariner, Mshauri Mkuu anayehusika na masuala ya mizozo wa shirika la Amnesty International alisema njia pekee ya kuukomesha mzunguko huu wa machafuko ni kuwachukulia hatua, kuwawajibisha na kuwaadhibu washukiwa. Mariner aliihimiza serikali ya Sudan Kusini ikomeshe unyanyasaji wa aina zote na kuianzisha mahakama maalumu ya uhalifu ambayo uundwaji wake umekwama tangu mwaka 2005.

"Tunaitaka serikali ya Sudan kusini iache juhudi za kukwamisha kuanzishwa kwa mahakama maalumu itakayosikiliza kesi za wahalifu wa kivita. Tungetaka serikali itie saini makubaliano kuhusu mahakama hiyo na iridhie mkataba wa kuundwa kwake. Muda umeshapita kwa washukiwa wa kesi za uhalifu wa kivita kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria."

Shirika la Amnesty International pia lililitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza azimio la vikwazo dhidi ya Sudan Kusini lililorodhiwa mnamo mwezi Julai mwaka huu.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/Amnestyinternational.org

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman