1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA yaipiga kalenda Euro 2020

Deo Kaji Makomba
17 Machi 2020

Shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA hatimaye limeahirisha michuano ya soka ya EURO 2020 hadi mwaka 2021 kufuatia mlipuko wa homa inayosababishwa na virusi hatari vya Corona.

https://p.dw.com/p/3ZaPd
Wegen Corona:UEFA EURO 2020 wird auf 2021 verschoben.
Kombe la EuroPicha: picture-alliance/dpa/F. Hoermann

Maafisa wa shirikisho hilo wamekubaliana kwa pamoja kuahirisha mashindano hayo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kuanzia Juni 12 hadi Julai 12 mwaka huu wa 2020, kwa mara ya kwanza katika nchi 12 mbalimbali barani humo.

Pendekezo la michuano hiyo kufanyika katika majira ya kiangazi mwaka 2021 limeungwa mkono na ligi ya taifa pamoja na Muungano wa vyama vya soka barani Ulaya, ECA, katika mkutano kwa njia ya vidio, ripoti kadhaa vya vyombo vya habari vimeeleza.

Shirikisho la kandanda la nchini Norway kupitia katika mitandao ya kijamii, lilisema kuwa UEFA inapanga mashindano hayo kufanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 11 mwaka 2021.

Mataifa wanachama 55 wa shirikisho hilo sasa wamekubali kuahirisha michuano hiyo katika mkutano mwingine uliofanyika kwa njia ya vidio, wenye maamuzi ya mwisho kutoka katika kamati kuu tendaji ya shirikisho hilo.

Rais wa shirikisho la kandanda barani Ulaya, Aleksander Ceferin aliandaa mkutano kwa njia ya vidio na wanachama wa UEFA, ECA, ligi za Ulaya na muungano wa wachezaji wa kulipwa, FIFPRO.

Bildergalerie Persönlichkeiten 2020 | Aleksander Ceferin
Rais wa UEFA Aleksander CeferinPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Tarantino

Baadhi ya viongozi wa ligi walishiriki katika mkutano huo huku wakiunga mkono kuahirishwa michuano ya EURO 2020, ambayo itavisaidia vilabu vyao kuongeza misimu yao.

Shirikisho la soka la nchini Italia, FIGC, na vilabu vya Serie A waliunga mkono kuahirishwa kwa michuano hiyo siku ya Jumatatu." Mabadiliko ya ratiba ni njia pekee ya kufuata kwa wakati huu," alisema kiongozi mkuu wa shirikisho la soka nchini Italia, FIGC, Gabriele Gravina, wakati akizungumza na shirika la habari la kitaifa, Ria Radio 1.

Michuano hiyo ya Euro 2020 ilikuwa imepangwa kufunguliwa mjini Rome Juni 12 na mechi zake kuendelea pia katika miji ya Munich, Amsterdam, Copenhagen, Bilbao, St Petersburg, Bucharest, Budapest, Baku, Glasgow, Dublin pamoja na London.

Kuenea kwa kasi kwa virusi vya Corona na kuwekwa vikwazo vya usafiri ambavyo kwa sasa vimewekwa na nchi mbalimbali ambapo kuahirishwa kwa michuano hiyo hakungeepukika.

Bado haijawa wazi ni kwanma gani kuahirishwa kwa michuano hiyo kwa kipindi cha miezi 12 itaathiri matukio mengine ya kimichezo hapo mwaka 2021. Huenda kukatokea mwingiliano wa michuano ya kombe la dunia la vilabu yanayoandaliwa na FIFA, ambayo inatarajia kufanyika China lakini iwapo tu hali ya kiafya itakuwa nzuri.

Ligi ya taifa ya UEFA pamoja na michuano ya vijana walio chini ya umri wa miaka 21 barani Ulaya pia imepangwa kufanyika katika kipindi kijacho cha majira ya kiangazi. Michuano ya mabingwa wa soka wanawake barani Ulaya imepangwa kufanyika England kuanzia Julai 7. Wanachama wa UEFA wanajadili pia ni kwa namana gani na michuano ya ligi soka barani humo, mashindano ya klabu bingwa ya mabara pamoja na ligi ya Ulaya.

Chanzo: DPA