Udhaifu wa kiraia unazima moyo wa kujenga jumuiya Tanzania | Matukio ya Afrika | DW | 18.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Udhaifu wa kiraia unazima moyo wa kujenga jumuiya Tanzania

Yako mambo mengi madogo madogo ambayo watu hutenda na kuleta mabadiliko. Lakini, kila wakati lazima pawepo msukumo ili kufanikiwa, iwe katika nyanja za elimu, afya bora, mazingira safi na mengineyo.

Hali ya mazingira wakati huu ina umuhimu zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na athari zake zisizofikirika katika maendeleo ya binadamu.

Wakati wanasayansi wanajadili uhusiano kati ya uunguzaji wa mafuta ya asilimwamba, kuongezeka kwa hewa ukaa na kupanda kwa halijoto duniani, Watanzania wanahitajika kuchukua hatua za haraka kurekebisha uharibifu mkubwa wa mazingira yao.

Ni zaidi ya miongo miwili tangu mfumo wa siasa za vyama vingi ulipoanzishwa Tanzania, lakini raia wa nchi hii bado si wepesi kuanzisha au kujiunga na vikundi vya hiari ambavyo vinaweza kuharakisha maendeleo na kuepusha mgogoro wa kimazingira ambao unaweza kutokea.

Shauku iliyoambatana na ushindi wa jumuiya za kiraia katika kuanzisha vyama vya siasa imefifia. Hata baadhi ya vyama vimepotea hivyo hivyo.

Lakini bado watu wanalalamika kuhusu ongezeko la umasikini; elimu duni; uhaba wa huduma bora za afya; unyanyasaji wa wanawake na watoto; ubaguzi wa kijinsia katika taratibu za kufanya maamuzi; ukosefu wa makazi bora; hali duni ya huduma za usafi wa mazingira na mambo mengine mengi katika mlolongo wa mapungufu katika maisha ya kila siku Tanzania.

Wakulima wadogo hawana imani tena na vyama vya ushirika. Katika mikoa ambapo vyama hivyo vilikuwa mhimili wa maendeleo kutokana na uuzaji wa mazao ya biashara hali imerudi nyuma baada ya kushuka kwa bei za mazao pamoja na uzalishaji.

Hali ni hiyo hiyo mijini ambako vyama vya ushirika wa walaji vilikuwa vimestawi kutokana na mafanikio ya kutetea haki za walaji na kuwasogezea bidhaa karibu. Wakati walaji wakiongezeka kila mwaka, vyama hivyo vimetoweka.

Mvua kubwa ziliponyesha wiki ya kwanza ya mwezi huu wa Mei katika ukanda wa pwani na kusababisha uharibifu uliotokana na mafuriko Dar es Salaam na Zanzibar, watu wengi walianza kutafakari wakijiuliza ni kitu gani kimevuruga mwenendo wa maisha. Zama zimepita ambapo jumuia zilijitoa kukabili changamoto kama hizo kabla ya kuomba msaada kutoka nje.

Kwa kiwango kikubwa mafuriko ya sasa ni changamoto kwa serikali kufanya matengenezo, kupanga na kujenga miundombinu inayofaa.

Maafisa wa serikali wamewaambia wakazi wa mabondeni ambayo hufurika wakati wa mvua wajijue wenyewe, kwa sababu mara kwa mara wamekaidi kufuata ushauri wa kuhamia sehemu za miinuko. Lakini waathirika pamoja na familia zao wanalia wapate msaada ambao haupatikani.

Wiki moja kabla ya mafuriko, wakazi wa mitaa ya Avocado, Kawe Beach and Mzimuni wilayani Kinondoni katika jiji la Dar es Salaam walitangazwa katika taarifa za televisheni kuwa ni mfano wa watu wanaojali kupendezesha mazingira yao.

Wana nia thabiti kutunza usafi wa mitaa, siyo tu kwa kuondoa taka lakini pia kuzuia madawa ya kulevya na uhalifu, vitu ambavyo vimeharibu sifa za maeneo mengi ya mijini na kuwanyima wananchi raha ya kujisikia kuwa na jumuiya zao wenyewe.

Wakati huo, mbunge wa jimbo la Ludewa kusini mwa Tanzania amefaulu kuwaunganisha wananchi, bila kujali vyama vyao vya siasa, wafanye kazi bila malipo kukamilisha mradi wa usambazaji umeme vijijini. Kwa kuwashawishi, ameweza kuwaongoza wafanye kazi ambayo italeta mabadiliko ya kudumu katika maisha baada ya vijiji vyao kupata umeme kutoka gridi ya taifa.

Hivyo basi kwa nini vikundi vya kiraia vilivyokuwa na mwamko zamani vimefifia baada ya demokrasia kuimarishwa? Kila mtu angetarajia kuona mwamko wa kiraia umeshamiri badala ya kufifia katika mfumo mpya wa kidemokrasia.

Kwa bahati mbaya, sivyo ilivyo. Jumuia nyingi zinakosa viongozi wa kuwashikia mwenge na kuwahamasisha ili watende mambo ambayo yataiwezesha nchi hii iwe mahali bora pa kuishi.

Mwandishi: Anaclet Rweyagura/ DW Dar es Salaam

Mhariri: Daniel Gakuba