1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVisiwa vya Comoros

Uchunguzi wa kifo cha aliyemshambulia Rais Azali wafungwa

Josephat Charo
26 Septemba 2024

Uchunguzi kuhusu kifo cha mwanajeshi aliyekuwa chini ya ulinzi mahabusu aliyemdunga kisu na kumjeruhi Rais wa Comoro Azali Assoumani umefungwa.

https://p.dw.com/p/4l6T6
Uchaguzi | Comoros | 2024 | Rais Azali Assoumani
Rais wa Comoro Azali AssoumaniPicha: REUTERS

Tangazo hilo lilitolewa jana Jumatano na mwendesha mashtaka wa umma mjini Moroni bila kutoa maelezo kuhusu jinsi alivyokufa.

Mwanajeshi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 24 alitiwa mbaroni mara tu alipomjeruhi Rais Assoumani katika shambulizi la kisu mnamo Septemba 13.

Mwanajeshi huyo alipatikana amekufa asubuhi iliyofuata katika chumba cha mahabusi alikokuwa akizuiliwa peke yake.

Soma pia:  Rais wa Comoro Azali Assoumani aapishwa kwa muhula wa nne

Taarifa ya afisi ya mwendesha mashitaka iliyochapishwa katika gazeti la serikali la Al-Watwan imesema wachunguzi walipofika kumhoji walimkuta amelala chini akiwa amekufa.

Ripoti inasema daktari wa jeshi alikadiria kifo kilitokea saa nane usiku na hakukuwa na majeraha kutokana na silaha wala vitu butu wala silaha zenye ncha kali. Taarifa inasema kutokana na haya afisi ya mwendesha mashitaka inachukulia hakuna sababu ya kufuatilia uchunguzi huu.