Uamuzi wa IOC wazusha hisia tofauti | Michezo | DW | 25.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Uamuzi wa IOC wazusha hisia tofauti

Urusi imeponea kupigwa marufuku wanariadha wake wote kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Rio kutokana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu. Lakini uamuzi huo wa IOC umezusha maoni tofauti

Uamuzi wa kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC wa kutowafungia wanamichezo wote wa Urusi kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Rio kuhusiana na mpango wa matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu uliofadhiliwa na serikali, umezusha hisia za mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa michezo ulimwenguni, ikiwa imebakia chini ya wiki mbili kabla ya sherehe ya ufunguzi.

Akizungumza ili kuhalalisha uamuzi wa jana, rais wa IOC Thomas Bach amesema marufuku ya jumla ingekiuka haki za wanariadha safi wa Urusi ambao wanataraji kushiriki katika Michezo hiyo ya Rio. "sasa hii haihusu matarajio, hii inahusu kuwatendea haki wanariadha safi kote ulimwenguni na katika njia hii tunawalinda wanariadha hawa safi kwa sababu ya vigezo vikali tulivyoweka kwa wanamichezo wote wa Urusi.

Schweiz Thomas Bach in Lausanne

Rais wa IOC Thomas Bach

Amesema mashirika binafsi ya michezo yatakuwa na jukumu la msingi kuamua kuhusu uhalali wa kila mwanamichezo wa Urusi kwenda Rio. Bach alisema kuna vigezo muhimu walivyoweka ili kutumiwa kabla ya kutoa idhini kwa kila mwanamichezo wa Urusi anayetaka kwenda Rio "kila binadamu anastahili haki ya kibinafsi. Tumeweka kiwango cha juu kabisa kwa namna wanamichezo wa Urusi wanaweza kupata fursa ya kwenda Rio. Wote wanastahili kutimiza kila mmoja idadi ya vigezo hivi vikali ambavyo tumeweka leo.

Waziri wa michezo wa Urusi Vitaly Mutko ameelezea matumaini kuwa wanariadha wengi wa Urusi wataweza kutimiza vigezo hivyo. "kuhusiana na vigezo vya kuiteuwa timu ya taifa ya Urusi katika mkesha wa Olimpiki, vigezo hivi bila shaka ni vikali lakini hii ni changamoto kubwa kwa timu yetu na nnaweza kusema kuwa nna uhakika kuwa wengi wa wanariadha wetu watatimiza vigezo hivyo.

Shirika la Kimataifa la Kupambana na Dawa zilizopigwa marufuku michezoni – WADA wiki iliyopita lilitoa wito kwa Urusi kupigwa marufuku baada ya kuorodhesha namna wizara ya michezo ya Urusi ilivyosimamia mpango mkubwa udanganyifu kwa msaada wa shirika la ujasusi la kitaifa.

Maafisa wa WADA wamesema wametamaushwa na umuzi huo wa IOC, ambao mkurugenzi mkuu Olivier Niggli amesema utasbabisha ukosefu wa uwianishaji, uwezekano wa changamoto na ulinzi mdogo wa wanariadha safi.

Mashirika 14 ya kitaifa ya kupambana na dawa za kuongeza misuli nguvu – ikiwemo Marekani, Ujerumani na Japan – pamoja na kamati kadhaa za kitaifa za Olimpiki zilitaka Urusi iondolewe katika michezo ya Rio.

Lakini kuna mengine yaliyounga mkono uamuzi wa IOC kama vile shirikisho la kimataifa la mchezo wa uogeleaji – FINA, na Chama cha kamati za kitaifa za Olimpiki zikisema unawapa nafasi wanariadha safi kushiriki michezo hiyo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga