Tunisia washerehekea miaka mitatu ya mapinduzi ya udikteta bila ya katiba mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Tunisia washerehekea miaka mitatu ya mapinduzi ya udikteta bila ya katiba mpya

Tunisia leo wameadhimisha mwaka wa tatu baada ya kuupindua utawala wa kidikteta nchini humo uliodumu kwa miongo kadhaa, ingawaje mgawanyiko wa misimamo ya kisiasa waliyonayo umesababisha kuchelewa kwa katiba mpya .

Mmoja wa raia aliyeshika bendera ya Tunisia,katika kusherehekea mapinduzi ya utawala wa kidikteta

Mmoja wa raia aliyeshika bendera ya Tunisia,katika kusherehekea mapinduzi ya utawala wa kidikteta

Rais Moncef Marzouki, waziri mkuu anayemaliza muda wake, Ali Larayedh, na aliyemteua kuchukua nafasi yake, Mehdi Jumaa, ni miongoni mwa viongozi kadhaa wa serikali waliohudhuria uzinduzi wa sherehe hizo za kumbukumbu ya tukio la mapinduzi dhidi ya udikteta, katika kitongoji cha Kasbah kilichopo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tuni), ambako pia ni makao makuu ya serikali.

Mojawapo ya shamrashamra hizo ni maandamano yaliyopangwa na Chama cha Ennahda katika mtaa wa Habib Bourguiba, kulipokuwa kituo cha raia waliokuwa katika mgomo wa siku kadhaa wakati wanaupinga utawala wa Zine El Abidine Ben Ali, waliyefanikiwa kumng'oa madarakani hapo tarehe 14 Januari 2011, baada ya kuwa amewatawala kwa mfumo wa kidikteta kwa miongo kadhaa.

Ulinzi mkali wakati wa sherehe

Polisi walisambazwa katika kila pembe ya mji huo kulinda doria. wa ajili ya kufanya doria ya usalama wa wananchi. Licha ya hamasa waliyokuwa nayo raia katika uzinduzi wa sherehe hizo, hofu pekee iliyokuwepo ni uchelewaji wa kuidhinishwa rasmi katiba yao mpya wanayoisubiri kwa hamu, ambayo ilitarajiwa kuwa tayari wakati wa sherehe hizo, lakini mpaka sasa bado inafanyiwa kazi.

Mtaa wa Bouguiba nchini Tunisia,kulipokuwa kambi ya raia walipogoma wakati wa mapinduzi ya Ben Ali

Mmojawapo ya mitaa iliyokuwa imefungwa kwa nyaya mjini Tunis

Katiba hiyo yenye vifungu 150, ambayo ni ya tatu kufanyiwa marekebisho, ilipaswa kuwa imekwishahakikiwa, baada ya mjadala wa wabunge kuhusu kuondoa baadhi ya vipengele uliochukua karibu wiki mbili, kukamilika.

Tunisia wataka raisi mwenye vigezo sahihi

Mojawapo ya vifungu vilivyopendekezwa kuwekwa ni ulazima wa kuwa na rais mwenye vigezo vinavyofaa, na uwepo wa mamlaka ya waziri mkuu. Pia wabunge wa nchi hiyo walipinga nafasi ya serikali kuteua majaji.

Raia wa Tunisia wanasubiri kuundwa kwa serikali mpya chini ya Jumaa, itakayosimamia nchi kuelekea uchaguzi mpya.

Waziri wa viwanda wa Tunisia, Mehdi Jomaa,aliyeteuliwa kuwa mrithi wa Waziri mkuu Ali Larayedh

Waziri wa viwanda wa Tunisia, Mehdi Jomaa,aliyeteuliwa kuwa mrithi wa Waziri mkuu Ali Larayedh

Uteuzi wa Jumaa wiki iliyopita, ulifanyika baada ya makubaliano ya kumaliza mvutano wa kisiasa kwa mwezi mzima, na kufuatiwa na maamuzi ya kuondoka madarakani kwa uongozi wa chama cha Kiislamu cha Ennahda, klichoshinda kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia baada ya mapinduzi ya umma dhidi ya dikteta Ben Ali.

Katika hotuba yake ya jana, Rais Marzouki alikiri kuwa viongozi wa serikali hawakuweza kukidhi matumaini makubwa ya kimageuzi waliyonayo wananchi miaka mitatu ya mapinduzi baada ya mapinduzi.

Mwandishi: Diana kago/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com