1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi aapishwa rasmi kuwa rais wa Congo

24 Januari 2019

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hii leo imemuapisha Felix Tshisekedi kuwa rais wake mpya, katika makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya amani katika taifa hilo tangu lipate uhuru karibu miaka 60 iliyopita.

https://p.dw.com/p/3C7MY
Demokratische Republik Kongo Kinshasa - Amtseinführung: Felix Tshisekedi wird Kongos Präsident
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Kiongozi wa upinzani, Felix Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55 na mtoto wa kinara wa upinzani marehemu Etienne Tshisekedi ameapishwa katika viwanja vya bunge mjini Kinshasa. Wafuasi wake ambao kwa miongo kadhaa walimuunga mkono baba yake Etienne, walifurika katika eneo hilo wakiwa wamechomeka bendera kwenye nyewle zao na kuvalia kofia na tai zenye chapa ya chui.

Matumaini ya Wakongo

Wakongo wengi wana mataumaini kwamba Tshisekedi ataleta mabadiliko baada ya miaka 18 ya utawala wa Rais Joseph Kabila, ambaye katika hotuba yake ya mwisho usiku wa Jumatano, aliihimiza nchi hiyo kuungana na kumuunga mkono kiongozi huyo mpya. Alisema alikuwa anaachia madaraka bila majuto yoyote.

Tshisekedi sasa ana jukumu la kushirikiana na bunge ambalo linadhibitiwa na wanachama wa muungano wa Kabila. Tshisekedi amekula kiapo akizungukwa na Kabila katika sherehe ilioungwa mkono na maelfu ya wafuasi ndani na nje ya jengo la bunge.

DR Kongo  Kinshasa Vereidigung Präsident Felix Tshisekedi
Rais anayeondoka madarakani, Joseph Kabila akimkabidhi uongozi Felix TshisekediPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa Desemba 30, 2019 ambao ulicheleweshwa mara tatu na matokeo yake bado yanapingwa na mgombea alieshika nafasi ya pili Martin Fayulu. Lakini Wakongo wengi wamekubali ushindi wa Tshisekedi kwa ajili ya amani.

Ahimiza maridhiano ya kitaifa

Katika hotuba yake baada ya kula kiapo, Tshisekedi amehimiza kuvumiliana, akitaja maridhiano ya kitaifa kuwa moja ya vipaumbele vyake.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na kiongozi mmoja tu wa nchi kutoka Afrika, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, baada ya Umoja wa Afrika na jumuiya ya kimataifa kueleeza wasiwasi kuhusu madai ya udanganyifu katika matokeo ya kura ambayo yalimpa ushindi Tshisekedi.

Marekani na mataifa mengine yalisema wiki hii kuwa watashirikiana na kiongozi huyo mpya, lakini hawakutuma salaam za pongezi. Ni wachache waliotarajia mpinzani kushinda uchaguzi nchini Congo, ambako Kabila aling'ang'ania kwa zaidi ya miaka miwili baada ya muhula wake kumalizika rasmi mwaka 2016.

Mwandishi: Iddi Ssessaanga
Mhariri: Caro Robi