Trump apanguwa tena timu yake ya mpito | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump apanguwa tena timu yake ya mpito

Rais Mteule Donald Trump apanguwa tena timu yake ya mpito kwa kuwaacha nje mtaalamu wa usalama na wapiga kampeni wake wa karibu akielekea kuwachaguwa watetezi wa soko la hisa la Marekani katika nyadhifa kuu za kiuchumi. 

USA Reince Priebus neuer Stabchef im Weißen Haus (Reuters/M. Segar)

Rais Mteule Donald Trump na Reince Priebus aliemchaguwa kuwa mkuu wa utumishi Ikulu.

Trump ambaye alipata ushindi wa kushtukiza wiki iliopita pia amevuka kikwazo cha urasimu ambacho kilikwamisha kwa muda uteuzi wa timu yake ya mpito baada ya kumwachia makamo wake wa rais mteule Mike Pence asimamie mchakato huo.

Trump ameandika katika mtandao wa Twitter kwamba mchakato ulioandaliwa vyema unafanyika wakati akiamuwa juu ya baraza lake la mawaziri na kwamba ni yeye tu ajuaye nani hatimae watakuwemo katika baraza hilo.

Walioko juu katika orodha yake kwa nyadhifa za kiuchumi ni mwenyekiti wa fedha wa kampeni na mwenye uzoefu mkubwa wa soko la hisa la Marekani Steve Muchin kama waziri wa fedha na mwekezaji aliekuwa akimuunga mkono kwa muda mrefu tajiri Willbur Smith kwa wadhifa wa waziri wa biashara.

Hata hivyo mwanachama wa Republikan maarufu Mike Rogers mwakilishi wa zamani wa baraza la wawakilishi la Marekani ambaye alitajwa kwa uwezekano wa kuwa mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA ameondoka kwa ghafla katika timu yake hiyo ya mpito.

Mawaziri wanaotegemewa 

Gedenkfeier USA New York 11. September (AP)

Rudy Giuliani meya wa zamani wa New York.

Watu waliokuwa watiifu kwa Trump kama meya wa zamani wa New York Rudy Guliani na balozi wa zamani wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa John Bolton wanafikiriwa kwa wadhifa wa waziri wa mambo ya nje.

Guliani meya wa New York wakati mji huo uliposhambuliwa na kundi la wanamgambo wa Al Qaeda Sep 11 mwaka 2001 anajulikana ni mtu mwenye msimamo mkali linapokuja suala la usalama wa taifa wakati Bolton ambaye ni mtu mwenye kupenda kutumia mabavu kwa masuala ya kigeni mwaka jana alisema Marekani inapaswa kuishambulia Iran kwa mabomu ili kuzuwiya mpango wake wa nyuklia.

Trump tayari amemteuwa Reince Priebus mtu wa ndani katika cha cha Republikan kuwa mkuu wa utumishi Ikulu na Steve Bannon kuwa mshauri wake mkuu uteuzi ulioshutumiwa na wanachama wa Demokrat,baadhi ya Warebuplikan na mashirika ya haki za binadamu.

Seneta Jeff Merkley amemtaka  Rais Mteule Trump kuondowa watetezi wa ubaguzi na chuki miongoni mwa viongozi wa utawala wake ni pamoja na kumtimuwa mara moja Steve Bannon kama mshauri mkuu.

Miongoni mwa viongozi wanaoukaribisha kwa matumaini utawala mpya waTrump ni pamoja na Rodrigo Duterte wa Ufilipino ambaye amesema amestahiki ushindi huo na Rais Bashar al Assad wa Syria aliesema anaweza kuwa mshirika halisi dhidi ya ugaidi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP
Mhariri :Gakuba Daniel
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com