1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Togo yamchagua rais mpya

4 Machi 2010

Nchini Togo uchaguzi wa rais umeanza rasmi hii leo utakaowashirikisha wapiga kura milioni 3 katika mtihani mkubwa wa demokrasia.

https://p.dw.com/p/MJOG
Rais aliye madarakani Faure GnassingbePicha: DW

Jumla ya wagombea saba wanawania wadhifa wa urais, akiwemo rais aliye madarakani, Faure Gnassingbe,pamoja na mwanamke wa kwanza kuwahi kuwania wadhifa huo, Brigitte Kafui Adjamagbo-Johnson wa chama cha Democratic Convention of African Peoples,CDPA.Jamii ya kimataifa inataraji kuwa shughuli ya leo itapita bila ghasia zozote ikikumbukwa kuwa maafa yalitokea katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2005. Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema hii leo kote  nchini humo. Kiasi cha zaidi ya wapiga kura milioni watatu wanashiriki katika uchaguzi huo wa rais. Jumla ya vituo 5930 vimefunguliwa mwendo wa saa nne asubuhi, saa za Afrika Mashariki, na vitafungwa baada ya muda wa saa kumi mwendo wa saa  mbili za usiku, saa za Afrika Mashariki.

Flash-Galerie Togo Wahlen
Wapiga kura waliopanga foleni mjini LomePicha: AP

Saini ya gumba

Mamia ya wapiga kura walipiga foleni katika shule moja ambayo inatumiwa kama kituo cha kupigia kura kwenye mtaa maarufu wa Pa de Souza ambao ni ngome ya upinzani iliyo karibu na eneo la ufukweni la mji mkuu wa Lome. Wapiga kura watalazimika kutia saini ya gumba ili kumchagua mgombea wanayemtaka.Tume huru ya uchaguzi ya Togo, CENI, imesisitiza kuwa kwa mara ya kwanza uchaguzi utakuwa  huru na wa haki, bila ghasia zozote.Kauli hizo zilitolewa na Rais wa Tume hiyo, Issifou Taffa Tabiou, aliyezungumza na waandishi wa habari. Kuna hofu kuwa ghasia huenda zikazuka kama ilivyotokea mwaka 2005.  

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja  wa Mataifa, kiasi cha watu 500 waliuawa katika ghasia zilizotokea wakati wa uchaguzi uliopita. Vifo hivyo vilitokea baada ya wafuasi wa chama cha  upinzani cha UFC kusababisha  vurugu kwa madai kwamba ushindi ulikuwa wao.Kwa sasa waangalizi wa Umoja wa Afrika na Ulaya pamoja na Jumuiya ya kibiashara ya mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, wanashiriki katika uangalizi wa uchaguzi huo.

Präsident Gnassingbe Eyadema - Togo
Hayati Rais Gnassingbe Eyadema,wa TogoPicha: AP

Hindi na Mchikichi

Rais aliye madarakani, Faure Gnassingbe, aliye na umri wa miaka 43 aliwahi kuwa waziri wa migodi na mshauri wa masuala ya fedha wakati marehemu babake alipokuwa madarakani. Kiongozi huyo anawania muhula wa pili wa rais. Marehemu babake, Gnassingbe Eyadema, aliiongoza Togo kwa muda wa miaka 38 bila ya pingamizi zozote kabla ya mwanawe Faure kumrithi.

Mpinzani mkuu wa Rais Gnassingbe ni Jean-Pierre Fabre wa chama cha Union Forces of Change,UFC, aliye na umri wa miaka 58. Chama chake ndicho chama  kikuu cha upinzani.

Chama tawala cha Togolese Peoples Rally,RPT, kilicho na nembo ya hindi kimekuwa madarakani kwa kipindi cha miongo minne chini ya uongozi wa Faure Gnassingbe. Chama kikuu cha upinzani cha UFC kilicho na nembo ya mchikichi kinaongozwa na Fabre ambaye ni mchumi.Kiongozi huyo wa upinzani tayari ameuelezea wasiwasi wake wa hila kufanyika ,´´Hakuna mtu ambaye anataka kuona uchaguzi ambao matokeo yake tayari yamekwishajulikana hata kabla ya kura kupigwa. Chama tawala cha RPT kitashindwa katika uchaguzi, lakini bado, hata hivyo, kitatangaza kuwa kimeshinda. Na hilo kamwe hatutoruhusu litokee. Hii ni hatari kwa sababu inaweza kusababisha ghasia´´,alifafanua

Ngome ya RPT

Eneo la Kara ndiyo ngome ya marehemu rais Gnassingbe lililo umbali wa kilomita 420 kaskazini mwa mji mkuu wa Lome. Akiwa katika eneo hilo, Faure aliwasihi raia wa Togo kudumisha amani kwani mshindi wa uchaguzi huo ni mmoja tu,  kwa hiyo hakuna haja ya kujihusisha na vitendo vya ghasia,''Sitoonyesha udhaifu katika kuwashughulikia wale watakaojaribu kuleta fujo, wakati wa kupiga kura au baada ya uchaguzi´´,alisisitiza.

Wakongwe na wapya wajitosa

Wagombea wengine wa wadhifa huo ni Waziri Mkuu wa zamani, Yawovi Agboyibo wa chama  cha Action Committee  for Renewal ,CAR, anawania wadhifa huo kwa mara ya tatu baada ya kushinda katika uchaguzi uliopita wa mwaka 1998 na 2003. Agboyibo aliye na umri wa miaka 67 ni mwanasheria na alizianza harakati za siasa mwaka 1990 baada ya ghasia za kisiasa kuzuka nchini humo. 

Mgombea mwengine wa upinzani ni Waziri mkuu wa  zamani Messan Abgeyome Kodjo wa chama cha Organisation for the Building of a United Togo,OBUTS,aliyejiondoa kwenye chama tawala cha RPT na kuunda chama chake mwaka 2005. Kodjo aliwahi kuwa Spika wa bunge la Togo katika kipindi cha mwaka 1999-2000 baada ya kushika nyadifa za uwaziri wakati wa utawala wa Eyadema. Hii ni mara ya kwanza anawania urais.

Mgombea wa kike pekee anayewania kinyang'anyiro hicho ni Brigitte Kafui Adjamagbo-Johnson wa chama cha Democratic Convention of African Peoples,CDPA.Bibi Johnson aliye mwanasheria ni mwanamke wa kwanza kuwahi kuwania wadhifa huo nchini Togo.

Mgombea wa urais kwa mara ya kwanza katika uchaguzi huu ni Bassabi Kagbara, mwalimu wa zamani wa chama cha Pan African Democratik pamoja na Nicolas Lawson wa chama cha Renewal  and Redemption,PRR.

Kampeni za uchaguzi zilizofanyika kwa amani zilihitimishwa Jumanne jioni hali ambayo ni tofauti na ilivyokuwa wakati wa uchaguzi uliopita wa mwaka 2005.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-RTRE/AFPE

Mhariri:  Miraji Othman