Teknolojia mpya kudhibiti wizi wa kura Kenya
4 Machi 2013Hatua hiyo ni jitihada nyingine ya kudhibiti vurugu kama za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 uliokumbwa na mzozo na kusababisha machafuko na vifo.
Waangalizi wa uchaguzi mara kwa mara katika chaguzi zilizopita wamekuwa wakiripoti wapiga kura bandia,masanduku ya kupigia kura kuwekwa makaratasi kabla ya uchaguzi na ukiukaji wa taratibu za uchaguzi. Lakini uchaguzi uliopita wa mwaka 2007 ndio uliokuwa mbaya zaidi kwani kulishuhudiwa umwagikaji damu huku karibu watu 1200 wakipoteza maisha yao baada ya wafuasi wa wagombea wawili wakuu kukabiliana.
Matumaini ya amani Kenya
Kenya haiwezi kurejea tena katika hali kama hiyo ya machafuko ya 2007 iliyosababisha taifa hilo linalosifika sana katika kanda hiyo ya Afrika mashariki kwa udhabiti wake wa kiuchumi kukwama na kuathiri pakubwa nyanzo za biashara za mataifa jirani. Wafadhili wa kutoka mataifa ya magharibi wana wasiwasi kuhusu Kenya,mshirika wao mkuu katika kanda hiyo hasa kuhusiana na vita dhidi ya makundi ya kigaidi.
Kipindi hiki,punde kura zitakapohesabiwa,matokeo kutoka kila kituo cha kupigia kura yatawasilishwa kwa tume ya uchaguzi kupitia njia ya kielektroniki na kuonyeshwa wazi kwa umma.Mfumo huo mpya ni kama ule uliotumika nchini Ghana katika uchaguzi wake mkuu mwaka jana,unaolenga kuondelea mbali makosa na kuzuia shutuma za udanganyifu.
Nafasi ya karatasi ya kupiga kura ipo
Bado kutatumiwa makaratasi ya kupigia kura ila wapigaji kura watatambuliwa kielektroniki. Simu zitakazotumika na maafisa wa uchaguzi katika vituo vya kupigia kura hazitakubali kutuma matokeo ambapo kura za jumla zinashinda zile zilizo kwenye sajili za wapiga kura wa eneo hilo. Hili la idadiya wapiga kura kutoingiliana na waliosajiliwa na tume ya uchaguzi lilikiwa suala lililozua malalamiko katika chaguzi zilizopita.
Wagombea wawili wakuu wa urais Raila Odinga na Uhuru Kenyatta ambao wamejiunga na wagombea wengine sita kutoa wito wa amani,walifanya mikutano yao ya mwisho ya kujipigia debe hapo jana Juamamosi mjini Nairobi kabla ya siku ya mwisho ya kampeini kukamilika.
Mikakati kabambe yawekwa
Mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Dismas Ong´ondi amesema wameweka mikakati kabambe wakati huu ili kuzuia yaliyotendeka wakati uliopita yasijirudie akiongeza kuwa watu huingiwa na taharuki iwapo matokeo yanachelewa kutangazwa akitaja hili kuwa mojawapao ya malalamishi yaliyochangia ghasia za mwaka 2007.
Kipindi hiki matokeo ya awali huenda yakatangazwa saa chache baada ya vituo kufungwa. Hata hivyo tume ya IEBC ina siku saba kuambatana na sheria kutangaza matokeo rasmi.
Wengi wa wapiga kura milioni 14 wana imani na mfumo huo mpya wa kutumia teknoljia licha ya kuwa wengine wanahofia huenda kukazuka tena ghasi baada ya uchaguzi. Vile vile wana imani na idara ya mahakama ambayo imefanya marekebisho makubwa na kuwa huru na haki na hivyo wataweza kukabiliana na mizozo itakayochipuka.
Mbali na kumchagua rais,wapigaji kura wa Kenya watawachagua magavana, maseneta,wabunge,wawaikilishi wa kaunti na wawakilishi wa wanawake.
Mwandishi: Caro Robi/ Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf.