1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IDEA: Yasema demokrasia imashakani kote duniani

2 Novemba 2023

Taasisi ya Kimataifa ya Demokrasia na Msaada wa Uchagizi IDEA iliyo na makao yake mjini Stockholm, Sweden, imesema katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba nusu ya nchi duniani zinakumbwa na mdororo wa demokrasia.

https://p.dw.com/p/4YJ5b
Uchaguzi wa Marekani 2020 mmoja ya waandamanaji Berlin, Ujerumani
IDEA Imesema kuna Ishara kwamba hata mataifa yaliyoendelea kidemokrasia, yanaanza kusonga nyuma katika hiloPicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Taasisi hiyo imesema masuala yanayochangia katika hilo ni chaguzi zisizo huru na ukandamizaji wa haki ikiwemo haki za kujieleza na mikusanyiko. Michael Runey ni mwandishi mwenza wa ripoti hiyo ya kila mwaka ya taasisi ya IDEA na amesema kuwa mwelekeo huu ambao ni kushuka kwa demokrasia katika kila kipimo cha demokrasia, unaathiri kila eneo duniani.

Runey ameongeza kuwa sio nchi zenye udikteta tu au nchi zilizopitia mapinduzi kaskazini mwa Jangwa la Sahara huko Afrika ndizo pekee zinazochangia kushukakwa demokrasia hiyo.

Amesema kwa sasa kunashuhudiwa pia kushuka kwa demomkrasia katika nchi ambazo kihistoria zimekuwa zikifanya vyema barani Ulaya na Asia."

Ripoti hiyo imesema mwaka 2022 ndio uliokuwa mwaka wa sita mfululizo ambapo idadi ya nchi zilizoshuhudia kushuka kwa demokrasia imezidi nchi zilizopiga hatua.

Taasisi hiyo inasema hicho ndicho kipindi kirefu zaidi cha kushuka kwa demokrasia ilichowahi kushuhudia tangu ilipoanza kuweka rekodi zake mwaka 1975.