1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taarifa ya Habari za Ulimwengu Asubuhi 25 Sept. 2016

Isaac Gamba
25 Septemba 2016

Umoja wa Ulaya wataka kusitishwa mapigano ya Aleppo, Polisi ya Charlotte, Marekani, yatoa vidio ya mauaji ya Mmarekani Mweusi, na mshukiwa wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) akamatwa nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2QZA4

Umoja wa Ulaya umesema mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia katika mji wa Aleppo kaskazini mwa Syria ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa juu ya ubinaadamu, ukitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzidisha juhudi za kurejesha amani nchini humo. Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, na Kamishina wa Masuala ya Kibinaadamu, Christos Stylianides, wamesema mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia ni jambo lisilokubalika, huku pia wakiyakosoa mashambulizi ya mabomu wiki iliyopita yaliyolenga kwa makusudi msafara wa magari yenye shehena ya misaada ya kiutu na pia kukatwa kwa huduma ya maji kwa raia walio wengi ambao bado wako katika mji huo wa Aleppo. Marekani inadai  msafara huo ulishambuliwa na ndege za kivita za Urusi ambayo inaendesha operesheni ya kijeshi ikiuunga mkono utawala wa Rais Bashar al-Assad. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema karibu raia milioni mbili wamekosa huduma ya maji katika mji huo wa kaskazini baada ya mashambulizi  ya mabomu yaliyofanywa na vikosi vya serikali kuharibu mtambo wa kusukuma maji. Wakati huo huo, Uingereza, Ufaransa na Marekani zimetoa wito wa kuitishwa kwa kikao cha haraka cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili juu ya kuendelea kwa mashambulizi katika mji wa Aleppo.