Sudan yakubali kuzungumza na S.Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 03.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Sudan yakubali kuzungumza na S.Kusini

Sudan imesema iko tayari kufanya mazungumzo ya amani na Sudan Kusini na imesema inatumaini nchi hiyo pia itaitikia wito wa Umoja wa Afrika unaozitaka zote kumaliza uhasama.

Rais Omar al-Bashir akizungumza na wanajeshi katika eneo la Heglig.

Rais Omar al-Bashir akizungumza na wanajeshi katika eneo la Heglig.

Hatua hii ya Sudan inafuatia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzitaka Sudan mbili kufikia muafaka ndani ya masaa 48 vinginevyo ziwekewe vikwazo.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari, wizara ya mambo ya nje ya Sudan imesema nchi hiyo iko tayari kushirikiana na timu ya wasuluhishi kutoka Umoja wa Afrika inayoongozwa na rais wa zamani wa Afrika kusini Thabo Mbeki. Msemaji wa wizara hiyo Al-Obeid Meruh amesema Waziri wake Ali Karti amethibitisha utayari wake kushiriki kikamilifu mchakato wa kurejesha amani kati ya nchi hizi mbili.

Baraza la Usalama latishia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya jumatano lilizitaka nchi hizo kuacha mapigano mara moja, na kila mmoja kuondoa vikosi vyake kutoka maeneo ya mwingine bila masharti yoyote, na kuweka usalama mipakani mwao ndani ya wiki moja, na kuacha mara moja matamchi ya uchochezi kupitia vyombo vya habari.

Jumanne iliyopita, Umoja wa Afrika uliliomba Baraza hilo kutilia mkazo matakwa yake kwa Sudan mbili kusitisha uhasama na kurudi kwenye meza ya mazungumzo ndani ya wiki mbili, na pia kufikia mwafaka ndani ya mizi mitatu.

Mhandisi wa Sudan akionyesha uharibu uliofanyika kwenye bomba la mafuta mjini Heglig.

Mhandisi wa Sudan akionyesha uharibu uliofanyika kwenye bomba la mafuta mjini Heglig.

China, Urusi zaunga mkono
Urusi na China ziliungana na wanachama wengine wa Baraza hilo kupitisha azimio linalounga mkono jitihata za umoja wa Afrika. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Suzan Rice alionya kuwa nchi hizi zilikuwa zinaelekea kwenye vita vikubwa ambavyo vinatishia amani ya kanda.

Sudan ilijiondoa kwenye mchakato wa amani ulioanzishwa na Umoja wa Afrika mwezi uliyopita baada ya Sudan Kusini kuvamia eneo la Heglig lenye utajiri mkubwa wa mafuta ambalo linatambulika kimataifa kama sehemu ya Sudan. Hatua hii ilifuatiwa na mashambulizi makubwa ya angani kutoka kwa Sudan na kutishia kutokea kwa vita vikubwa baina ya nchini hizi.

Uhasama baina ya nchi hizi ulizidi baada ya kutengana Julai mwaka jana kutokana na kuwepo masuala kadhaa ambayo hayajapatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na umiliki wa maeneo yenye utajiri wa mafuta, mgawanyo wa mapato yatokanayo na mafuta na madai ya kila upande kuwa upande mwingine unaunga mkono waasi wake.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Sudan Kusini yaomba kusaidiwa
Waziri wa Sudan Kusini anayehusika na mausala ya Baraza la Mawaziri, Deng Alor Kuol alisema nchi yake iko tayari kufuata matakwa ya Umoja wa Mataifa lakini akaomba msaada wa haraka kwa waathirika wa mashambulizi ya Sudan.

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Daffa-Alla Elhag Ali aliliambia Baraza la Usalama kuwa amani kati ya Sudan mbili itapatikana tu kwa Sudan Kusini kuacha aina zote za msaada na hifadhi kwa waasi wanaopambana na Sudan.

Umoja wa Afrika ulisema siku ya Jumatano jioni kuwa Sudan ilitoa taarifa rasmi kuufahamisha utayari wake kushiriki mazungumzo. Tayari Sudan Kusini ilishaonyesha utayari wake kuzungumza na Sudan na sasa mataifa hayo yana muda hadi Jumanne ijayo kuanza tena mazungumzo, na miezi mitatu kufikia muafaka.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman