1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan kumkabidhi Omar al-Bashir ICC

11 Agosti 2021

Waziri wa mambo ya nje amesema Sudan itamkabidhi aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, pamoja na maafisa wengine wanaoshukiwa kuhusika na mzozo wa jimbo la Darfur.

https://p.dw.com/p/3yqvt
Sudan Präsident Omar al-Bashir
Picha: Reuters/M. N. Abdalla

Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Mariam al-Mahdi amesema Sudan itamkabidhi aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, pamoja na maafisa wengine wanaoshukiwa kuhusika na mzozo wa jimbo la Darfur uliogharimu maisha ya watu 300,000 na kuwaacha wengine milioni 2.5 bila makaazi. 

Waziri al-Mahdi amenukuliwa na chombo cha habari cha serikali akisema kuwa baraza la mawaziri limeamua kwa sauti moja kuwakabidhi maafisa wanaoshukiwa kuhusika na mzozo wa Darfur katika mahakama ya ICC.

Soma zaidi: Mfumuko wa bei waongezeka zaidi nchini Sudan

Uamuzi huo uliafikiwa wakati wa ziara ya mwendesha mashitaka-mkuu wa mahakama ya ICC Karim Khan nchini Sudan. Agina Ojwang, wakili na mchambuzi wa siasa za kimataifa kutoka Nairobi anasema hakutarajia uamuzi huo.

Bashir, aliyeiongoza Sudan kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu kabla ya kuondolewa madarakani kufuatia maandamano makubwa ya mwaka 2019, anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika jimbo la Darfur.

Umoja wa Mataifa unasema watu 300,000 waliuawa na wengine milioni 2.5 walipoteza makaazi yao katika mzozo wa jimbo la magharibi la Darfur mnamo mwaka 2003. Ghasia ziliibuka baada ya waasi, ambao ni Wasudan weusi kulalamikia juu ya ubaguzi wa kimfumo katika serikali iliyotawaliwa na Wasudan wenye asili ya kiarabu. Serikali ya Khartoum ilijibu kwa kuwatuma wanamgambo wa Janjaweed kupambana na wapiganaji wa makabila ya watu weusi.

Bashir, mwenye umri wa miaka 77 amekuwa akisakwa na mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi tangu mwaka 2009 baada ya ICC kutoa agizo la kukamatwa kwake.

Bashir aliondolewa madarakani kufuatia maandamano makubwa ya mwaka 2019

Sudan Khartum | Anti-Regierungsproteste
Waandamani katika mji mkuu wa Khartoum Picha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Sudan inaongozwa na serikali ya mpito inayojumuisha raia na jeshi tangu Agosti mwaka 2019, serikali hiyo imeahidi kuwatendea haki wahanga wa uhalifu uliofanywa chini ya utawala wa Bashir.

Ilitia saini makubaliano ya amani mnamo mwezi Oktoba na makundi ya waasi katika jimbo la Darfur, wakati baadhi ya viongozi wa makundi hayo ya waasi wakichukua nyadhifa za juu serikalini japo ghasia zinaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.

Soma zaidi: Ruzuku za petroli na dizeli zasimamishwa Sudan

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamemshtumu Bashir na wasaidizi wake wa zamani kwa kufanya ukatili ikiwemo ubakaji, mauaji, uporaji na hata kuchoma vijiji.

Mwaka uliopita, kiongozi mwandamizi wa kundi la wanamgambo la Janjaweed Ali Muhammad Ali Abd al-Rahman alijisalimisha katika mahakama ya ICC.

Majaji wa ICC walisema mnamo mwezi Julai kuwa kiongozi huyo mwandamizi atakuwa mshukiwa wa kwanza kupandishwa kizimbani juu ya mzozo wa Darfur, akikabiliwa na mashitaka 31 yakiwemo mauaji, ubakaji na kutesa watu kinyama.