Suala la askari watoto laiponza Rwanda | Matukio ya Afrika | DW | 04.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Suala la askari watoto laiponza Rwanda

Marekani imetangaza kuiwekea vikwazo Rwanda na nchi nyengine kadhaa kwa kuhusika katika matumizi ya askari watoto jambo ambalo limekanushwa na Rwanda kuwa inawasaidia waasi wa M23 wenye kutumia askari watoto huko Congo.

Askari watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Askari watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwa masuala ya Afrika Linda Thomas-Greenfield amesema kwamba Marekani inaitumia Sheria ya nchi hiyo ya Kuwalinda Askari Watoto,kwa kuiwekea vikwazo Rwanda ikiwa ni juhudi za serikali ya Marekani kukomesha uandikishaji wa watoto jeshini.Hata hivyo amesema wataendelea kuwa na mazungumzo na serikali ya Rwanda juu ya suala hilo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Marie Harf amesema Rwanda inawekewa vikwazo hivyo kwa sababu ya kuliunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo linaendelea kuwaandikisha watoto jeshini na kuwateka nyara na kwa hiyo kutishia utulivu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kundi la M23 linalodhibitiwa na waasi wa Kitutsi ambao walikuwa wanajeshi wa zamani wa Congo walianza kuteka sehemu za mashariki ya Congo hapo mwaka jana kwa kuituhumu serikali kwa kushindwa kutimiza makubaliano yao ya amani ya mwaka 2009.

Harf amesema Rwanda haitopatiwa msaada wa kifedha wa kijeshi wa kimataifa kutoka Marekani kusaidia masuala ya elimu na mafunzo jeshini. Pia haitopatiwa msaada wa kugharamia majeshi ya kigeni unaohusu mauzo ya zana za kijeshi za Marekani na huduma za kijeshi.

Yapinga kuwajibishwa na matukio ya Congo

Kundi la waasi wa M23 wakiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kundi la waasi wa M23 wakiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Rwanda imesema kwamba tuhuma kuwa inalisaidia kundi la waasi wa M23 nchini Congo lenye kutumia askari watoto hazina ushahidi wa msingi.Brigedia Generali Joseph Nzabamwita msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda amesema nchi yake haipaswi kuwajibishwa na matukio yalioko nje ya udhibiti wake. Amesema inashangaza kwamba Rwanda iwajibishwe kwa mambo ambayo hayatokei kwenye ardhi yake na wala haiyatendi. Ameendela kusema kwamba ikiwa kama mshirika wa muda mrefu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda serikali ya Marekani ina ushahidi wa kutosha kwamba vikosi vya Rwanda katu havikuwahi kuvumilia matumizi ya watoto katika mapambano.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani vikwazo hivyo pia vimewekwa kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Myanmar,Sudan na Syria lakini haiko wazi iwapo nchi hizo zinapata msaada wa kijeshi wa Marekani.

Lengo kukomesha matumizi ya askari watoto

Askari mtoto akiwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Askari mtoto akiwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Serikali ya Marekani imesema lengo lao ni kushirikiana na nchi zilizoorodheshwa kuhakikisha ukomeshaji wa aina yoyote ile ya kuhusishwa kwa askari watoto na kuandikishwa jeshini.

Nchi nyengine tatu ambapo majeshi yao yanajulikana kwa kuwaandikisha na kuwatumia askari watoto ambazo ni Chad, Sudan Kusini na Yemen zimeondolewa vikwazo vya kijeshi vya Marekani kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake.Na kwa ajili ya maslahi ya Marekani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Somalia zimeondolewa kwa kiasi fulani vikwazo hivyo vya kijeshi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul -Rahman