Steinmeier ziarani Irak | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Steinmeier ziarani Irak

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amekutana na viongozi wa Irak akiwa Baghdad kwa ziara ya siku mbili ambayo haikutangazwa hapo kabla.

In this photo released by the Iraqi Government, Iraqi President Jalal Talabani, left, meets Frank-Walter Steinmeier, the German foreign minister in Baghdad, Iraq, Tuesday, Feb. 17, 2009. (AP Photo/Iraqi Government) ** EDITORIAL USE ONLY **

Waziri Frank-Walter Steinmeier(kulia) akikutana na Rais Jalal Talabani.

Steinmeier ni Waziri wa Nje wa kwanza wa Ujerumani kuitembelea Irak tangu1987.Ziara hiyo iliwekwa siri hadi dakika ya mwisho kwa sababu za usalama.Lakini ziara ya Steinmeier inashangaza pia upande wa kisiasa, kwani waziri huyo anatoa ishara mpya-jambo ambalo wala halikutegemewa muda mfupi kabla ya kumalizika kipindi cha serikali ya hivi sasa mjini Berlin. Ikiwa ni miaka sita tangu serikali ya kansela wa zamani Gerhard Schroeder kupinga vita vya Irak,sasa Ujerumani inataka kuisaidia serikali ya Baghdad kuijenga upya Irak kama anavyoeleza waziri Steinmeier:

"Serikali mpya imeshika madaraka Marekani.Na nchini Irak kuna dalili kuwa hali ya usalama inakuwa bora.Ninaamini kuwa huu ni wakati mwafaka kutazama ikiwa Ujerumani inaweza kusaidia kazi za kuijenga upya Irak."

Wanadiplomasia wa Ujerumani mwishoni mwa mwaka 2008 walisema, waziri wa mambo ya nje ataizuru Irak kama ishara ya kumuunga mkono Rais wa Marekani Barack Obama,alieahidi kuharakisha utaratibu wa kuondosha vikosi vya Marekani kutoka Irak.Kwa hivyo,ziara ya Steinmeier mjini Baghdad inatazamwa kama ni ishara ya kukaribiana na serikali mpya ya Marekani.

Steinmeier amekwenda Irak akiwa na mapendekezo mbali mbali ya msaada kushirikiana katika sekta za afya,utamaduni na elimu.Mbali na mikutano yake na Waziri Mkuu wa Irak Nuri al Maliki,Rais Jalal Talabani na waziri mwenzake wa nje Hoshyar Zebari,Steinmeier vile vile amepanga kukutana na wajumbe wa makanisa na Waziri wa Haki za Binadamu.Majadiliano hayo yatahusika na masuala ya kiutu na hali ya wakimbizi. Wairaki wapatao kama milioni 4 walilazimika kukimbia makwao na wanaishi katika kambi za wakimbizi nchini Syria na Jordan.Kufuatia jitahada za Ujerumani,Umoja wa Ulaya umesema upo tayari kuwapokea wakimbizi 10,000 wa Kiiraki. Ujerumani nayo itawapatia makaazi mapya Wairaki wa Kikristo wapatao 2,500.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amefuatana na wajumbe wa ngazi ya juu wa kampuni kubwa za Kijerumani.Kwa mfano tawi la Siemens linalohusika na nishati na kampuni inayohusika na vifaa vya hospitali German Medical Care.Waziri Mkuu wa Irak, Nuri al-Maliki amezialika kampuni za Kijerumani kuwekeza katika Irak mpya,bila kujali msimamo wao kuhusu uvamizi wa Irak.

 • Tarehe 17.02.2009
 • Mwandishi S.Überbach - (P.Martin) AFPE
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GwGm
 • Tarehe 17.02.2009
 • Mwandishi S.Überbach - (P.Martin) AFPE
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GwGm
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com