1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia: Waziri mkuu amtuhumu Rais kuingilia uchunguzi

Angela Mdungu
8 Septemba 2021

Waziri mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble leo, amemtuhumu Rais Mohamed Abdullahi Mohamed kuingilia uchunguzi muhimu unaohusu hatma ya jasusi wa nchini humo ambaye kupotea kwake kulizua mjadala mkali nchini humo

https://p.dw.com/p/4049p
Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed | Farmajo
Picha: Str/AFP

Ikran Tahlil, afisa katika Shirika la intelijensia na usalama wa taifa NISA, mwenye umri wa miaka 25 alitekwa nyara karibu na nyumbani kwake mjini Mogadishu mnamo mwezi Juni. Juma lililopita, waajiri wake walitoa taarifa kuwa alitekwa nyara na kuuwawa na wanamgambo wa Al-shabaab

Katika hali isiyo ya kawaida, kwa haraka wanamgambo hao walikanusha kuhusika, wakati familia ya Tahlil ikilituhumu shirika la usalama wa taifa NISA kwa kumuuwa jasusi huyo, mtazamo unaoungwa mkono na raia wengi wa Somalia ambao wameigeukia mitandao ya kijamii kuilaani taasisi hiyo na kutaka haki itendeke.

Jumapili iliyopita, waziri mkuu Roble alimfuta kazi mkurugenzi wa shirika la ujasusi Fahad Yasin baada ya kuiita ripoti ya shirika hilo kuwa "haiaminiki", lakini mkurugenzi huyo alirejeshwa kazini na Rais Mohamed Abdullahi Mohamed siku iliyofuata. Rais Mohamed Abdullahi Mohamed anayejulikana pia kama Farmajo, alisema kufutwa kazi kwa mkuu huyo wa NISA kulikuwa kinyume cha sheria na katiba.

Matendo ya Farmajo yanaathiri uchunguzi

Hali ilipamba moto Jumatano baada ya  Rais Farmajo kumpandisha cheo Bwana Fahad Yasin kuwa mshauri wa usalama wa taifa, hali inayotishia kulipuka kwa mgogoro wa kisiasa katika taifa hilo ambalo tayari halina utulivu.

Waziri mkuu Mohamed Hussein Roble amesema, matendo ya Rais yanaathiri uchunguzi wa kupotea kwa Tahlil "kwa namna ile ile ambayo haki na vyombo vya sheria vimekuwa vikizuiwa kufanya uchunguzi kamili katika siku za nyuma" amesema, hali hiyo ni hatari  kwa mfumo wa utawala wa taifa hilo.

Roble, ambaye alipewa jukumu la kuratibu uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu ili kuyazima maandamano baada ya Rais Farmajo kujiongezea muda wa utawala bila uchaguzi, alimtuhumu pia Rais kwa kujaribu kujibebesha majukumu ya uchaguzi na ya kiusalama kutoka kwake.

Somalia Ministerpräsident Mohamed Hussein Roble
Waziri mkuu wa Somalia Mohamed Hussein RoblePicha: Somalian Presidency/AA/picture alliance

Roble aliteuliwa na Farmajo kuwa waziri mkuu Septemba mwaka uliopita, lakini wawili hao wamekuwa wakikwaruzana katika miaka ya hivi karibuni  jambo linalotishia kuuhatarisha mchakato wa uchaguzi. Jumuiya ya kimataifa tayari inawasiwasi huku Umoja wa Mataifa, Ujumbe wa Umoja wa mataifa nhini Somalia (AMISOM), Marekani, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya nchi za mashariki na Pembe ya Afrika IGAD, zikiwataka viongozi hao wa Somalia washughulikie tofauti zao haraka iwezekanavyo.

Taarifa iliyotolewa na ujumbe wa umoja wa mataifa nchini Somalia mapema Jumanne ulisema "Tunawataka viongozi wa Somalia wapunguze msuguano wa kisiasa unaozunguka uchunguzi huu, na hasa, waepuke vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha machafuko".

Uchaguzi wa bunge wa Somalia, unatarajiwa kufanyika Oktoba 1 na Novemba 25 baada ya kucheleweshwa kwa muda mrefu. Katika uchaguzi huo wabunge na wajumbe wa koo mbalimbali humchagua Rais.