Sierra Leone kutoa uchambuzi wa mwanzo juu ya Ebola | Matukio ya Afrika | DW | 04.11.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Sierra Leone kutoa uchambuzi wa mwanzo juu ya Ebola

Wafanyakazi wa afya nchini Sierra Leone, wametoa ripoti mpya ya uchambuzi wa mwanzo juu za ugonjwa hatari wa Ebola. Ripoti hiyo inaonesha ni sababu gani zinazopelekea kupona kwa baadhi na wengi wengine hupoteza maisha.

Dousseyni Daou Hospital in Kayes Mali Ebola Kind

Wafanyakazi wa Afya wa ugonjwa wa Ebola

Ripoti hio iliyotoka siku ya Jumatano (29.10.2014), inajumuisha uchunguzi wa wagonjwa 106 waliyoathirika na ugonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Serikali ya Kenema huko Sierra Lione. Uchunguzi huo ulifanyika baina ya tarehe 25 Mei hadi tarehe 18 Julai.

Madaktari 47 waliongoza uchunguzi huo, ambao sita kati yao walifariki kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa jambo linaloweza kutathmini kama mgonjwa aliyeathirika na Ebola ataweza kunusurika, ni idadi ya virusi vilivyozaliana katika damu ya mgonjwa huyo kabla ya kuanza matibabu.

Kwa mfano, katika uchunguzi huo wagonjwa waliyokuwa ni kiasi ya virusi milioni 10 kwa kila mililita ya damu, walifariki kwa asilimia 94. Ikilinganishwa na vifo vya asilimia 33tu, vya wagonjwa waliyokuwa na virusi kiasi ya 100,000 kwa kila mililita ya damu.

Halikadhalika lengine lililowekwa wazi na utafiti huo ni kwamba; vijana wanaweza kuhimili ugonjwa wa Ebola zaidi kuliko wazee. Hili linathibitishwa na takwimu zinazosema kuwa, zaidi ya asilimia 94 ya vifo ni vya wagonjwa waliopindukia miaka 45 ikilinganishwa na asilimia 57 ya vifo vya vijana walio chini ya miaka 21.

Dalili juu ya ugonjwa wa Ebola

Uthibitisho juu ya dalili za ugonjwa huo umeonesha homa ndio dalili ya awali, na ndio dalili inayonekana kwa wagonjwa wengi. Lakini pia hufuatiwa na mgonjwa kuumwa na kichwa, kupoteza nguvu za mwili, kusikia kizunguzungu, kuharisha, kupata maumivu makali sehemu za tumbo, pamoja na kutapika.

Symbolbild - Ebola

Mwanasayansi wa ugonjwa wa Ebola

Zaidi ripoti hiyo imesema kuwa wagonjwa wanaonesha dalili za kupoteza nguvu za mwili, kusikia kizunguzungu na kuharisha wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupoteza maisha.

Alisema kiongozi wa utafiti huo, Dk. John Schieffelin, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza wa Chuo Kikuu cha Tulane kuwa

“ Kuharisha kunakotokana na ugonjwa wa Ebola ni jambo hatari sana. Kwavile hali hio husababisha kupotea kwa maji na chumvi za mwili, na tiba kubwa ni kurejesha yale maji yaliyopotea.”

Aliongeza kwa kusisitiza, madaktari lazima wawe waangalifu na hilo.

Katika uchunguzi huo pia imeonekana huchukua baina ya siku 6 hadi 12, mpaka virusi vya ugonjwa huo kujitokeza katika damu ya mgonjwa. Na pale dalili zilipojitokeza, basi asilimia 74 kati ya wagonjwa hao 106 waliochaguliwa kufanyiwa uchunguzi walifariki dunia.

Umuhimu wa uchambuzi wa kisanyansi

Schieffelin alisema uchambuzi huo utaleta ufahamu wa kina juu ya ugonjwa wa Ebola. Ambao utawasaidia wafanyakazi wa afya kukabiliana kwa tahadhari zaidi na wagonjwa walioathirika, na pamoja na kurahisisha kupatikana kwa matibabu mapya.

Ingawa kuna baadhi ya watafiti walidadisi matumizi ya fedha zilizotumika kuuchunguza ugonjwa huo wa Ebola. Badala yake walishauri kuwa fedha hizo zingetumika kusaidia kukabiliana na janga hilo moja kwa moja.

Ripoti hiyo tayari imeshawekwa kwenye mtandao wa intaneti, na inapatikana katika gazeti la utabibu la New England.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/APE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman