′Sera ya misaada ya Marekani imechoka′ | Masuala ya Jamii | DW | 19.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

'Sera ya misaada ya Marekani imechoka'

Wachambuzi wanasema sera ya msaada wa kigeni ya Marekani imepitwa na wakati na sasa wanapendekeza yafanyike mageuzi yatakayozingatia uwajibikaji na majukumu zaidi kwa mataifa yanayopokea msaada huo.

Hayo ni kwa mujibu wa waraka wa kisera uliotolewa hivi karibuni na mtandao wa maboresho ya msaada ya kigeni MFAN, ambao ni muungano wa watetezi wa maendeleo ya kimataifa na wataalamu wa sera ya nje. Waraka huo ulibainisha kuwa msaada ni kielelezo muhimu cha majukumu ya kimaadili, kiuchumi na kiusalama ya Marekani, na kwamba taifa hilo linaendelea kuwa mfadhili muhimu zaidi, lakini msaada wa Marekani umekosa uwazi na ufanisi.

Mkurugenzi wa ufanisi wa misaada katika shirika la hisani la Save the Children Sylvain Browa, aliliambia shirika la habari la IPS kuwa Marekani inahitaji kubuni na kutoa misaada katika namna ambayo ingeweza kusaidia ufanisi wa misaada kwa kushirikiana na mataifa husika ili kupata matokeo endelevu.

Marekani inatoa misaada hata kwa mataifa yaliyo na uchumi mkubwa kama China, kama inavýoonyesha katika picha hii.

Marekani inatoa misaada hata kwa mataifa yaliyo na uchumi mkubwa kama China, kama inavýoonyesha katika picha hii.

Wadau wapya

Browa alisema katika mazingira yanayobadilika, ambako msaada wote unaendelea kuwa muhimu katika kunusuru maisha, kutibu magonjwa na kuwapeleka watoto shuleni, wadau wapya wanaibuka, na hawa wanawahusisha viongozi wenyeji na wananchi wanaojua zaidi vipaumbele vyao.

Kwa mujibu wa faharasi ya uchangiaji wa maendeleo ya mwaka 2013, Marekani ilishika nafasi ya 17 kati ya wafadhili wakuu 22, katika ubora wa msaada unaotolewa. Kila mwaka, faharasi hiyo inayaorodhesha mataifa tajiri kulingana na namna yanavyowasaidia maskini katika nyanja za msaada, biashara, fedha, uhamiaji, mazingira, usalama na teknolojia.

Kwa mujibu wa safu hiyo, ni shirika moja tu la Marekani lililopewa alama ya "nzuri sana" katika kipengele cha uwazi. Shirika linalohusika na sehemu kubwa ya msaada wa Marekani la USAID lilipata kiwango cha "sawa" tu, wakati wizara ya mambo ya kigeni na programu ya kupambana na ukimwi PEPFAR zilipewa alama ya "mbaya" na "mbaya sana."

Uwajibikaji na umiliki

MFAN inapendekeza kuwa sera mpya iliyoboreshwa, na kujengwa kwa nguzo za uwajibikaji na umiliki wa mataifa, inaweza kuboresha ufanisi wa msaada wa kigeni wa Marekani. Taarifa ya MFAN ilisema bila kutoa kipaumbele kwa nguzo hizo mbili, nchi hiyo itarejea mfumo wa zamani uliochoka, na ambao unaendeleza utegemezi wa misaada.

Magari ya wagonjwa yaliyotolewa na USAID kwa Afghanistan.

Magari ya wagonjwa yaliyotolewa na USAID kwa Afghanistan.

Programu mpya imesanifiwa kuziwezesha jamii, na hatimaye kuleta umiliki wa kitaifa wa miradi ya maendeleo, anasema George Ingram, mwenyekiti mwenza wa MFAN na mwanataaluma mwandamizi katika taasisi ya ushauri ya Brookings ya nchini Marekani.

Mapendekezo haya yameungwa mkono na makundi mengine ya maendeleo. Casey Dunning, mchambuzi wa sera katika kituo cha maendeleo ya dunia cha nchini Marakani pia, alisema waraka huo una umuhimu mkubwa kwa mashirika yote ya misaada, watekelezaji na wenye kufikiri.

Lakini alionya kuwa kulikuwepo na ugumu pia katika mapendekezo yake, hasa katika maana nzima ya umiliki wa mataifa na ni mambo yepi yanaendana na uwajibikaji. Alisema mashaka katika tafsiri na vipimo vya uwajibikaji na umiliki wa mataifa yanaleta ugumu wa kuufanya msaada kuwa na ufanisi.

Hata hivyo, ripoti ya MFAN inasaidia kuweka vigezo vya kujenga uwezo na kuona hasa nini hicho kinachomaanisha. Browa kutoka Save the Children pia anabainisha kuwa dhana zilizoainishwa katika ripoti siyo mpya vile. Lakini anaongeza kuwa zikiwekwa pamoja, zinaweza kusaidia kujenga uwezo wa wenyeji na kuweka umiliki wa rasilimali na zana za maendeleo.

Msaada wa chakula wa Somalia.

Msaada wa chakula wa Somalia.

Mapendekezo

MFAN inapendekeza kuwa ili kuwa na uwazi zaidi, serikali ya Marekani inapaswa kutekeleza kikamilifu viwango vipya vya uwazi - International Aid Transparency Initiative IATI kufikia mwishoni mwa mwaka 2015. Pia Faharasi ya uwazi katika utoaji wa misaada inapaswa kupelekwa katika mashirika yote ya Marekani, jambo ambalo kwa sasa halifanyiki.

Zaidi ya hayo, mashirika yote ya Marekani yanapaswa kuanza kutoa taarifa za kifedha katika mtandao wa taarifa za serikali, maarufu kama Foreign Assistance Dashboard, na mwisho maamuzi ya misaada ya maendeleo yanahitaji kuongozwa na tathmini kubwa.

MFAN inasema kwa pamoja, uwazi na tathmini vitayasaidia mashirika hayo kupata matokeo bora kwa walipa kodi wa Marekani na pia jamii zinazopokea msaada wa Marekani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ips
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com