1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaRwanda

Rwanda yaanza zoezi la kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa mpox

20 Septemba 2024

Rwanda imeanza kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa mpox kwa kutumia dozi 1,000 iliyopokea kutoka Nigeria chini ya makubaliano kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/4ksTo
DR Kongo Kabare | Kavumu-Krankenhaus Patient mit Mpox Verdacht
Muuguzi akichukua sampuli kutoka kwa mgonjwa anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa kupooza katika hospitali ya Kavumu eneo la Kabare, jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Hayo yamesemwa jana na kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa barani Afrika, Afrika CDC.

Daktari Nicaise Ndembi kutoka kituo cha Afrika CDC amefahamisha kuwa zoezi hilo la kutoa chanjo lilianza mnamo siku ya Jumanne na lililenga wilaya saba zenye "watu walio katika hatari kubwa” wanaoishi kwenye mipaka jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Nigeria ilitoa dozi 1,000 kwa Rwanda kutoka kwenye mgao wa dozi 10,000 ambazo ilipokea kutoka Marekani.

Soma pia: Kongo yapokea chanjo zaidi za ugonjwa wa Mpox kutoka Marekani

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa kitovu cha mlipuko wa ugonjwa wa mpox barani Afrika ambapo wagonjwa wapya 2,912 na vifo 14 vimeripotiwa katika muda wa wiki moja iliyopita, na kupelekea idadi jumla ya wagonjwa wa mpox kuwa 6,105 na vifo 738 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

"Lazima tuzuie mlipuko wa ugonjwa wa mpox haraka sana,” amesema mkurugenzi mkuu wa kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa barani Afrika, Afrika CDC Daktari Jean Kaseya.

Kaseya ameeleza kuwa Rwanda na nchi nyingine zimetoa wito wa kutolewa kwa dozi zaidi tofauti na ya walizozihitaji awali. Wataalamu wa afya barani Afrika wamekadiria kuwa bara hilo litahitaji takriban chanjo milioni 10 ili kuzuia mlipuko wa mpox.

Serikali ya Japan imesaini makubaliano na serikali ya Kongo kutoa dozi milioni 3 za chanjo dhidi ya mpox.