Rwanda, Mauritania zathibitisha kesi za kwanza za Corona
14 Machi 2020Wizara ya afya ya taifa hilo la Afrika ya kati limesema katika taarifa leo(14.03.2020) kwamba mtu huyo alikuwa anaonesha ishara za ugonjwa huo wakati alipowasili nchini Rwanda akitokea katika mji wa Mumbai nchini India hapo Machi 8. Taarifa ya wizara hiyo imesema Machi 13 mtu huyo alifika mwenyewe katika kituo cha afya ambako mara moja alifanyiwa uchunguzi na sasa yuko katika hali nzuri.
Taifa la Afrika magharibi la mauritania limethibitisha kesi ya kwanza ya virusi vya corona mtu huyo akiwa mgeni ambaye aliingia nchini humo Machi 9 akitokea barani Ulaya. Waziri wa afya Mohamd Nazir Ould Hamid amesema jioni Ijumaa kuwa mgonjwa "aliondolewa mara moja na hatua zote za kiafya zimechukuliwa kumtibu na kudhibiti kesi hiyo ya kwanza ya virusi vya corona nchini humo."
Virusi vya corona vinasambaa katika nchi nyingi za Afrika. Kenya , Guinea na Ethiopia zimeripoti kesi zao za kwanza siku ya Ijumaa, wakati Gabon na Ghana zimefanya hivyo jioni ya Alhamis. Sudan pia imeripoti kesi ya kwanza ya muathirika wa virusi vya corona ambaye amefariki.
Nchi 19 kati ya 54 barani Afrika zimeripoti kesi za virusi vya corona. Maafisa wanasema nyingi ya kesi hizo ni kutoka mataifa ya kigeni.
Baada ya kujifungia ndani chini ya sheria nchini Italia ya kutoruhusu watu kutembea ovyo nchi nzima ili kupambana na virusi vya corona, mamilioni ya Wataliani wameamka leo Jumamosi wakijikuta wamenyimwa moja ya burudani ya kawaida iliyobaki, kutemea katika maeneo nje ya nyumba zao.
Sehemu za wazi za michezo zafungwa
Meya ya miji , ikiwa ni pamoja na Roma na Milan, waliamua ilipofika jioni ya Ijumaa kufunga sehemu za kucheza watoto pamoja na maeneo ya wazi. Maafisa wa afya wamelalamika kuwa watu wengi mno wanajikusanya pamoja, iwapo ni kucheza mpira, ama kufanya mazowezi ya kukimbia katika makundi.
Chini ya amri ya serikali iliyotolewa mapema wiki hii, watu waliruhusiwa kufanya matembezi, kufanya mazowezi wa kukimbia ama kuendesha baisikeli katika maeneo ya wazi iwapo tu watakaa mbali mbali kati ya mtu na mtu. Lakini hakuna mtu aliyetekeleza sheria hiyo.
New Zealand, Cambodia na Taiwan ni miongoni mwa nchi katika eneo la Asia Pacific kutangaza vizuwizi vipya vya usafiri siku ya Jumamosi kama sehemu ya juhudi za dunia kuzuwia kusambaa kwa virusi vipya vya corona.
Kila mtu anayeingia New Zealand kuanzia kesho Jumapili itabidi atengwe kwa muda wa siku 14, waziri mkuu Jacinda Ardern amesema katika mkutano na waandishi habari. Ameongeza kuwa ni wasafiri tu kutoka katika kisiwa hicho cha bahari ya Pacific ambao hawatahusika na sheria hiyo.
Amewataka raia wa New Zealand kuepuka safari ambazo si lazima nje ya nchi na kusema meli za safari za watalii hazitaruhusiwa kutia nanga katika bandari za nchi hiyo hadi Juni 30.
Uhispania inajitayarisha kutangaza hali ya hatari leo Jumamosi (14.03.2020) na Italia inaimarisha hatua yake ya kuwazuwia watu kutoka majumbani mwao kwa kufunga maeneo ya burudani ya wazi, wakati Denmark na Poland zimekuwa nchi za hivi karibuni kufunga mipaka yao kwa wasafiri katika juhudi za kupunguza kasi ya kusambaa kwa virusi vipya vya Corona.