1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Rudolf Bell: Mfalme wa Cameroon aliyepinga ukoloni

Yusra Buwayhid
14 Februari 2021

Mfalme Rudolf Douala Manga Bell wa Cameroon alisoma Ujerumani na kuupenda sana ustaarabu wa taifa hilo. Lakini baadae alikosana nao pale wakoloni wa Kijerumani walipoanza kuwanyanyasa watu wake. Mwishowe, walimnyonga.

https://p.dw.com/p/3pJwg

Rudolf Manga Bell: Mfalme wa Cameroon aliyesimama dhidi ya ukoloni wa Ujerumani

Rudolf Douala Manga alikuwa nani?

 Rudolf Douala Manga Bell alizaliwa mwaka 1873 mjini Douala, Cameroon. Alikuwa ni mjukuu wa Mfalme Ndumbe Lobe Bell – ambaye pia akijulikana kama Mfalme Bell – aliyesaini Mkataba wa Hifadhi na Himaya ya Ujerumani mnamo mwaka 1884.

Rudolf Douala Manga Bell alikwenda kusoma Ujerumani kabla ya kurudi nyumbani ambako wakati huo kukiitwa "Kamerun” na kumsaidia baba yake kuongoza Ufalme wa Douala. Alimpokea madaraka Septemba 2, 1908.

Kwanini Rudolf Douala Manga Bell alikosana na Ukoloni wa Ujerumani?

Mfalme Doula Manga alijifunza sheria ya Ujerumani wakati akipopata fursa ya kufanya kazi kwenye utawala wa kikoloni wa Ujerumani ulipochukua udhibiti wa nchi yake. Kuna wanaosema alisoma sheria ya Ujerumani katika Chuo Kikuu cha Bonn, Ujerumani. Lakini baadae alipoteza heshima juu ya sheria hiyo baada ya kugundua kuwa wakoloni hao walikuwa hawafuati kanuni za sheria yao wenyewe. Baada ya miaka miwili ya utawala, Waduala wenzake walimteua kuongoza mapigano ya kuwapinga wakoloni wa Ujerumani kuendelea kukamata ardhi yao, kitu ambacho, Mfalme Douala Manga alisema, ni ukiukaji wa mkataba uliotiwa saini na babu yake.

Zeichnung African-Roots-Beitrag
African Roots: Rudolf Douala Manga Bell

Mjini Douala wakati huo, Wazungu na Waafrika walikuwa wakiishi kwenye mitaa miwili tofauti. Wajerumani walitaka kujitenga na Waafrika na hasa kuwazuia wasiingine mtaa wao wa Plateau Joss (ijulikanayo sasa kama Bonanjo, wilaya ya utawala ya Douala) kwa sababu wakiogoba wasije kuwaambukiza ugonjwa wa Malaria.

Vipi Rudolf Douala Manga Bell aliongoza mapigano hayo?

Rudolf Douala Manga Bell alianzisha kundi lilokuwa likiendesha harakati zake katika maeneo ya ndani. Aliweza kuanzisha mtandao wa wafuasi uliokuwa na washirika ndani ya

eneo la "Kamerun”. Harakati zake za mapigano pia zilipata usaidizi kutoka chama cha Social Democrats katika bunge la Ujerumani ambacho siasa zake zikiunga mkono kwa watu kuweza kujitawala wenyewe.

Kutokana na kwamba alisoma katika shule na vyuo vikuu vya Ujerumani, alijaribu kutumia njia za kisheria alizojifunza akiwa nchini humo. Lakini alipogunduwa kwamba mikakati ya kisheria haikuwa ikimsaidia, aliamua kuitisha maandamano ya umma Douala.

Zeichnung African-Roots-Beitrag
Asili ya Afrika: Rudolf Douala Manga Bell

Kifo cha Rudolf Douala Manga Bell kilitokeaje?

Wajerumani walitaka kudhibiti kila aina ya uasi kulipozuka Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1914. Utawala wa Ujerumani ulimfungulia mashtaka Rudolf Douala Manga Bell baada ya kumkamata Agosti 7, 1914, na kumhukumu kifungo cha maisha kwa makosa ya uhaini.

Usiku wa siku hiyo, Kanali Zimmermann alimpa ruhusa ya kwenda kuiaga familia yake. Rudolf Douala Manga Bell angetaka angekimbia, lakini aliamua kurudi gerezani siku ya pili ili kukabiliana na hukumu yake ya kifo. Agosti 8, mfalme huyo wa Doual aliuliwa kwa kunyongwa.

Maneno yake ya mwisho yalikuwa ni haya: "Mnanyonga damu isiyo na makosa. Munaniua bure. Na matokeo yake yatakuwa makubwa sana.”

Wakameroon wanamkumbukaje Rudolf Douala Manga Bell?

Anakumbukwa kama mtu aliyekufa shahidi kwa nchi yake na aliyesimama dhidi ya wakoloni wa Kijerumani. Baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba uasi ulioanzishwa na Manga Bell ndiyo uliokuja kuzaa vuguvugu la kupigani uhuru wa Cameroon.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.