1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto milioni 280 duniani kote wana maisha bora

Sylvia Mwehozi
29 Mei 2019

Ripoti kuhusu hali ya watoto duniani iliyochapishwa na shirika la wahisani linaloshughulikia haki za watoto la Save the Children inaonyesha maendeleo makubwa katika sekta za afya, elimu na usalama katika nchi kadhaa.

https://p.dw.com/p/3JN8i
Save the Children - Uganda Schule in in Nakasongola
Picha: Andrew Pacutho/Save the Children

Save the Children imesema katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba hali ya maisha ya watoto duniani imeimarika katika jumla ya nchi 173 kati ya 176, ambazo ilizifanyia utafiti. Angalau watoto milioni 280 duniani kote wana maisha bora ukilinganisha na ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.

Hata hivyo ripoti hiyo inaonyesha kwamba robo ya watoto duniani kote bado wananyimwa haki ya usalama na kufurahia utoto, ambapo wengi bado wanakimbia makazi yao au kukwama katika nchi zilizo na mizozo.

Singapore inashika nafasi ya juu katika viwango vya ulinzi na huduma kwa watoto, ikifuatiwa na mataifa manane ya Ulaya ikiwemo Ujerumani pamoja na Korea Kusini. Katika nafasi ya mwisho ziko nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Mali na Sudan Kusini licha ya kushuhudiwa maendeleo katika miaka ya karibuni.

Niger ni mojawapo ya nchi iliyopiga hatua kubwa katika kuboresha maisha ya watoto ndani ya miongo miwili iliyopita ikifuatiwa na Rwanda, Sierra Leone, na Ethiopia.

Syrien Krieg - Kinder
Watoto waliokimbia vita huko SyriaPicha: Getty Images/AFP/Z. Al Rifai

Marekani ipo nafasi ya 36 katika ripoti ya mwaka huu ikiwa sawa na China. Mkurugenzi wa shirika la Save the Children Carolyn Miles alisema ripoti hiyo ilizingatia viashiria vinane vya ukuaji wa mtoto ikiwa ni pamoja na mtoto kunusurika, elimu, ajira za watoto na ndoa za mapema ukilinganisha na mwaka 2000. "Kumekuwa na maendeleo mazuri ukiangalia duniani kote", alisema mkurugenzi huyo. 

Aidha kiasi ya watoto milioni 420 wanaishi katika maeneo yaliyo na mizozo duniani kote hiyo ikiwa ni mara mbili ya idadi ya mwaka 1995 na takribani watoto milioni 31 hivi leo wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Ripoti hiyo iliyotolewa kuelekea siku ya mtoto duniani ambayo ni Juni mosi, inakadiria kuwa jumla ya watoto milioni 690 wanaporwa utoto wao kutokana na maradhi, vifo, ndoa za utotoni, mimba za mapema, utapiamlo au kushindwa kuhudhuria shule.

Ukilinganisha na mwaka 2000, vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua kwa asilimia 49, ajira za watoto asilimia 40, utapiamlo sugu na ndoa za utotoni. Ripoti hiyo inasema kati ya viashiria vinane vilivyotumika, kiashiria kimoja kimeonekana kuchomoza zaidi ambacho ni idadi ya watoto wanaoishi katika maeneo yenye mizozo au walioathiriwa na vurugu.

AP/AfP