Randrianirina aapishwa kuwa Rais wa Madagascar
17 Oktoba 2025
Katika hafla iliyofanyika katika Mahakama ya Juu ya Katiba mjini Antananarivo, Kanali Michael Randrianirina amekula kiapo chake akisema:
"Nitatimiza kikamilifu, kwa ukamilifu na kwa haki majukumu makubwa ya nafasi yangu kama Rais wa Jamhuri ya Madagascar." Naapa kwamba nitatekeleza mamlaka niliyopewa na nitatoa nguvu zangu zote kulinda na kuimarisha umoja wa kitaifa na haki za binadamu."
Awali, Randrianirina alitangaza kuwa jeshi limechukua madaraka na kuvunja taasisi zote isipokuwa Bunge la Kitaifa. Alieleza kuwa kamati inayoongozwa na jeshi itatawala kwa kipindi cha hadi miaka miwili sambamba na serikali ya mpito, kabla ya kuandaa uchaguzi mpya.
Maandamano ya Gen Z yachochea mabadiliko ya uongozi
Randrianirina alikuwa kamanda wa kikosi maalum cha CAPSAT, ambacho kilihusika katika mapinduzi ya mwaka 2009 yaliyomleta Andry Rajoelina madarakani. Hata hivyo, wiki iliyopita alijitenga na Rajoelina, akiwahimiza wanajeshi wasiwafyatulie risasi waandamanaji.
Wakati vijana wengi wakishangilia kuanguka kwa utawala wa Rajoelina, baadhi yao wameanza kuonyesha wasiwasi kuhusu kasi ya jeshi katika kujaza nafasi ya uongozi.
Rajoelina, ambaye alikimbilia nje ya nchi mwishoni mwa wiki, aliondolewa madarakani na wabunge, lakini amekataa kujiuzulu licha ya maafisa wengi wa usalama kujiondoa upande wake.
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zalaani mapinduzi
Umoja wa Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, wameyalaani mapinduzi hayo, ambayo yametokea baada ya wiki kadhaa za maandamano ya kizazi cha "Gen Z".
Maandamano hayo, yaliyoanza mwezi uliopita, yanafanana na harakati za vijana wa Gen Z katika Nepal, Sri Lanka na maeneo mengine. Vijana wa Madagascar walianza kuandamana kupinga kukatika mara kwa mara kwa maji na umeme, lakini baadaye wakaanza kuibua masuala mengine kama vile gharama ya maisha, ukosefu wa fursa, na tuhuma za ufisadi na upendeleo miongoni mwa viongozi wa juu.
Madagascar ina idadi ya watu takriban milioni 30, ambapo robo tatu ya watu wanaishi katika umasikini. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, kati ya mwaka wa uhuru 1960 hadi 2020, pato la taifa kwa kila mtu liliporomoka kwa asilimia 45.