1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kommentar

Abdu Said Mtullya5 Januari 2012

Rais wa Ujerumani, Christian Wulff, ataendelea katika wadhifa wake baada ya kujaribu kujitetea katika mahojiano na televisheni, lakini mhariri mkuu wa DW, Ute Schaeffer, anasema Wulff anaendelea kuwa rais wa majaribio!

https://p.dw.com/p/13eea
Rais Christian Wulff katika mahojiano na ARD/ZDF.
Rais Christian Wulff katika mahojiano na ARD/ZDF.Picha: Reuters

Rais Wulff ameepuka kujiuzulu lakini jee ameirejesha imani? Alijaribu kuyatimiza mambo hayo mawili katika mahojiano ya televisheni. Yumkini ameweza kuepuka kujiuzulu angalau kwa sasa, lakini kuhusu kurejesha imani, mambo yatakuwa magumu. Uungaji mkono kwa Rais huyo unatoweka. Ni kutokana na kutambua hilo kwamba alitokea katika televisheni wakati inatazamwa na watu wengi. Alikiri kutenda makosa.

Alisema njia aliyoitumia katika kulikabili suala la mkopo haikuwa nzuri kwa ofisi yake. Pia alisema jinsi alivyowatishia wandishi wa habari kuwa watakiona, kwa sababu tu ya kufanya uchunguzi juu yake, haukuwafiki na dhima yake kama Rais.

Kuhusu masuala fulani Wulff alijizonga mwenyewe. Kwa mfano juu ya uhusiano wake na wafanyabiashara na juu ya kwenda likizo kwa kuitumua mifuko ya wafanya baishara hao wakati alipokuwa waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxoy la kaskazini magharibi mwa Ujerumani. Wulff amesema hakuvunja sheria yoyote. Alijitokeza kwa unyenyekevu na alijitahidi kuonyesha kwamba mushkeli uliotokea unatokana na udhaifu wa mwanadamu.

Kwa ufupi, hapakuwa na mengi mapya katika aliyoyasema na juu ya tathmini ya mikasa iliyotokea. Ndiyo maana, hata baada ya mahojiano, bado palikuwa na maswali mengi yanayopaswa kujibiwa. Kwa mfano, je Wulff anacho kifua cha kuyazuia madhara zaidi yanayoweza kuiathiri ofisi ya rais? Je, bado anayo matumaini kama waliyokuwanayo wananchi juu ya wadhifa anaopaswa kuuwakilisha?

Mhariri wa gazeti la Bild, Nikolaus Blome.
Mhariri wa gazeti la Bild, Nikolaus Blome.Picha: picture-alliance/dpa

Mtu anaweza kuwa na mashaka juu ya hayo. Chembelecho hata wale wanaosema aendelee na kazi yake walitarajia kumwona Rais huyo akijokosoa mwenyewe - yaani kiongozi aliyewahi kusema hadharani kwamba yeyote anayetaka kuwamo katika sehemu ya uongozi anapaswa kutimiza wajibu wa kuwa mfano wa kuigwa kwa moyo wote.

Wadhifa wa urais siyo mahala panapostahili kufanyia mafunzo kama ambavyo alivyowahi kusema mwenyewe Wulff. Dhima kuu kama ya urais inapaswa kuwakilishwa kwa mifano ya uadilifu na yule anayeibeba. Yeyote anayejitokeza kama kiongozi wa familia na mwanachi mwadilifu, anapaswa kuishi kulingana na maadili hayo.

Ndiyo sababu ni jambo la kushangaza zaidi kuona makosa yaliyofanywa na Wulff. Kwa nini amekuwa anatoa habari nusu nusu juu ya mkopo aliopewa wakati alipokuwa waziri mkuu? Kwa nini aliwatishia waandishi wa habari kwa kujaribu kuzuia uchunguzi wao na kuacha ushahidi katika kinasa sauti cha simu?

Rais Wulff alisema hivi karibuni kwamba yeyote anayejihesabu kuwa miongoni mwa viongozi wenye mamlaka, hawezi kujitenga na kuishi katika dunia ya peke yake. Hayo yana maana malumu kwa rais. Hata ikiwa sasa, baada ya mahojiano atataka kufirikia vingine, Wulff atabakia kuwa Rais aliyekuwamo katika majaribio!

Mwandishi: Ute Schaeffer/DW
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Saumu Yusuf