1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zweifel an Wulff

Mohammed Khelef5 Januari 2012

Jana (04.01.2012), Rais Christian Wulff wa Ujerumani alifanya mahojiano na waandishi wa habari juu ya kashfa ya mkopo wa nyumba na pia simu aliyopiga kwa gazeti la Bild kulikemea kwa kuchapisha kashfa hiyo mwaka jana.

https://p.dw.com/p/13ebX
Rais Christian Wulff akiwa katka mahojiano na vituo vya ARD na ZDF.
Rais Christian Wulff akiwa katka mahojiano na vituo vya ARD na ZDF.Picha: dapd

Jambo kubwa katika mahojiano hayo ni ukweli kuwa Rais Wulff aliomba radhi ingawa amekataa kujiuzulu. Lakini hata kabla ya kufanyika kwa mahojiano hayo ya jana, tayari wanasiasa wa upinzani walishayatolea maoni, kama kwamba walikisia kile ambacho kingelisemwa na Rais Wullf.

Marina Weisband, ambaye ni kiongozi wa chama kipya cha Piraten, alisema kwamba Wulff amekuwa akitumia fursa ya kuwapo kwake ofisini kujinufaisha, tangu alipokuwa waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony la Kaskazini Magharibi mwa Ujerumani.

Weisband aliyatuma maoni hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, akihoji kwamba mazungumzo ya Rais Wulff na waandishi wa habari, yalikuwa yameandaliwa tu kumsafisha rais huyo mwenye kashfa.

Baada tu ya kufanyika kwa mahojiano hayo ya dakika 20, kiongozi wa chama cha CSU bungeni, Gerda Hasselfeldt, alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, kutokuziaibisha ofisi wanazozitumikia. Lakini kiongozi wa chama cha CDU, ambacho kimo katika muungano na chama cha CSU, Ruprecht Polenz, alisema kwamba Rais Wullf hajatenda kosa.

Kiongozi wa CDU bungeni, Ruprecht Polenz.
Kiongozi wa CDU bungeni, Ruprecht Polenz.Picha: picture-alliance/ dpa

"Ninachokiona ni kuwa tunalazimika kumuachia Rais Wulff kutekeleza wajibu wake, kwa sababu mpaka sasa hakujakuwa na ushahidi wowote kwamba ametenda kosa." Alisema Polenz.

Katibu Mkuu wa CDU, Hermann Gröhe, alisema alichokiona katika dakika zile 20 za mahojiano yaliyorushwa na vituo vya televisheni vya ARD na ZDF, ni kiwango cha juu cha uwazi na uwajibikaji cha Rais Wulff, akiongeza kwamba ana hakika kwamba baada ya mahojiano hayo, Rais Wulff atakuwa ameweza kurejesha imani ya raia kwake.

Lakini imani ya upinzani kwa Rais Wulff haikurejeshwa na mahojiano haya. Ingawa hadi sasa chama kikuu cha upinzani, SPD, kimejaribu kutoa maoni yake kwa tahadhari.

"Mahojiano yameacha maswali wazi. Suala lililopo ni ikiwa ofisi ya raisi wa shirikisho inaweza kukaliwa naye au kuachwa. Suala ni ikiwa alipokuwa waziri mkuu wa Lower Saxony alifanya kosa la jinai au la. Na bado linabakia suala la jumla la namna gani rais wa shirikisho anaweza kwenye vyombo vya habari na kuonesha tu kwamba yote yaliyopita, ndiyo yawe yamepita tu." Amesema kiongozi wa SPD bungeni, Hubertus Heil.

Katibu Mkuu wa SPD, Hubertus Heil.
Katibu Mkuu wa SPD, Hubertus Heil.Picha: dpa

Gazeti la Bild liliripoti kwa mara ya kwanza tarehe 13 mwezi Disemba, kwamba Rais Wulff alipokea mkopo binafsi wa Euro lakini tano kutoka kwa mke wa mfanyabiashara na rafiki yake mkubwa, Egon Geerkens, alipokuwa waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony la kaskazini magharibi mwa Ujerumani.

Wabunge wa vyama vya upinzani katika jimbo hilo waliuliza iwapo Wulff alikuwa na uhusiano wa kibiashara na Geerkens, na Wulff alijibu hakuwa na uhusiano huo, lakini hakutoa taarifa juu ya mkopo aliopewa. Tayari maafisa wa idara ya sheria wamesema hawaoni iwapo pana ushahidi wowote juu ya kutendeka kosa la jinai kuhusu mkopo huo.

Itakumbukwa kuwa, Rais Wulff anayetokea chama cha CSU, alipendekezwa kushikilia wadhifa huo na Kansela Angela Merkel, na ndiyo maana wengi wanaona kuwa kashfa inayomkabili sasa, inamuathiri pia Kansela Merkel. Akizungumza msimamo wa Kansela Merkel baada ya mahojiano ya jana, msemaji wake, Georg Streiter, amesema bado Kansela ana imani na Rais Wulff.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Georg Streiter.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Georg Streiter.Picha: picture alliance/dpa

"Kansela wa Serikali ya Shirikisho ana imani kamili na Rais Wulff, kwamba anaweza kutumukia vyema wajibu wake. Ameweza kuyajibu kwa ufasaha maswali aliyoulizwa na Kansela Merkel ana matumaini kwamba ataendelea mbele zaidi." Amesema Streiter.

Lakini wakati Kansela Merkel akiliunga mkono chaguo lake, ukosoaji mkali zaidi kuliko wote umetoka kiongozi wa chama cha die Linke, Gesine Lötzsch, ambaye ameyaita majibu ya Rais Wulff kwa waandishi wa habari "yanayofadhaisha."

Mwandishi: Mathias Bölinger
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo